MSEMAJI Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, ametoa taarifa za mafanikio ya serikali; ambayo ni pamoja na Watanzania 300,000 kuchangamkia chanjo, kuongezeka kwa makusanyo ya Mamlaka ya Mapato (TRA), ununuzi wa ndege tano na kupunguza gharama za kipimo cha haraka cha corona.
CORONA
Msigwa alisema tayari idadi hiyo ya Watanzania 300,000 wamepatiwa chanjo huku virusi vya corona, serikali ikitangaza kuanza utaratibu wa kuwafuata wananchi mahali walipo kuwapatia chanjo kwa hiari hasa maeneo ya vijijini.
Hadi sasa vituo zaidi ya 550 vinatumika kutoa chanjo kwa wananchi katika maeneo mbalimbali, tangu mpango huo ulipozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Julai 28 mwaka huu, Ikulu, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, Msigwa alisema serikali itaanza utaratibu wa kuwafikia Watanzania hususan vijijini kuwapatia chanjo.
“Nasisitiza zoezi hili ni hiari, anayetaka kuchanjwa akachanje, afya ya mtu ni jukumu lako binafsi. Ukiumwa utakwenda hospitali utakuwa unapumua kwa msaada wa mashine peke yako. Ningependa Watanzania tuwasikilize wataalamu,” alisisitiza.
BEI YA VIPIMO VYA CORONA YAPUNGUZWA
Msigwa alisema serikali imechukua hatua katika maeneo yaliyokuwa yalilamikiwa hususan gharama za vipimo vya corona mipakani ambapo changamoto hizo zimetatuliwa.
“Katika mipaka yetu, wananchi wanapimwa kipimo cha haraka bila kulipia. Na hii inafanyika ili kurahisisha biashara na shughuli zingine za wananchi,” alifafanua.
Aliongeza kuwa: “Palikuwa na malalamiko ya gharama za vipimo kwa wasafiri waendao nje ya nchi hasa katika viwanja vyetu vya ndege, lakini sasa tatizo hilo limetatuliwa kwa kupunguza gharama za kipimo cha haraka.”
Alisema kipimo hicho cha haraka kimepunguzwa kutoka dola 25 hadi dola 10 na kipimo cha PCR kimepunguzwa kutoka dola 100 hadi dola 50.
Alitoa wito kwa Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya corona kwa sababu ugonjwa huo upo, unawaathiri watu na kusababisha vifo.
WATUMISHI WA DARASA LA SABA
Akizungumzia agizo la serikali lililotolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuhusu watumishi wa darasa la saba walioondolewa kazini mwaka 2017, Msigwa alisema baadhi ya vyombo vya habari vilimnukuu vibaya Waziri Mkuu.
Alisema uhalisia wa agizo hilo ni kwamba, watumishi 4,380, waliorudishwa kazini ni wale ambao waliajiriwa serikalini kabla ya mwaka 2004 wakiwa na sifa ya darasa la saba.
Katika agizo hilo, alisema Waziri Mkuu aliagiza wakurugenzi wa halmashauri kuwasilisha orodha ya watumishi ambao wana sifa ya kurudishwa kazini ili ifanyiwe kazi.
“Si kweli kwamba Waziri Mkuu kaagiza watumishi walioondolewa kazini kwa vyeti feki warudishwe kazini kama inavyoelezwa,” alisisitiza.
SEKTA YA ELIMU
Kwa upande wa elimu, alieleza katika mwaka huu wa fedha serikali iliamua kuongeza bajeti katika mikopo ya elimu ya juu kutoka sh. bilioni 464, mwaka uliopita hadi kufikia sh. bilioni 570.
Msigwa alisema kumekuwa na ongezeko idadi ya wanafunzi wanufaika na mikopo hiyo kutoka 149,398 hadi kufikia wanafunzi 160,000.
“Tangu kufunguliwa kwa dirisha la mikopo mwaka huu hadi Agosti 27 wanafunzi 88,694 wameomba mikopo na wengine wanaendelea kuomba hadi mwisho wa dirisha la mikopo Agosti 31 mwaka huu.
MAKUSANYO YA MAPATO
Kuhusu mapato, alisema serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa mwezi imekusanya sh. trilioni 1.535 sawa na asilimia 97.4 ya lengo iliyojiwekea kukusanya kwa kipindi cha Julai mwaka huu.
Makusanyo hayo ni makubwa ikilinganishwa na makusanyo ya Julai mwaka jana, ambapo ilikusanya sh. trilioni 1.284, sawa na asilimia 84.1 ya lengo.
Msigwa, alisema ongezeko hilo la makusanyo halihusiani na tozo za miamala ya simu.
“Serikali inawapongeza Watanzania kwa kuendelea kuitikia wito wa kulipa kodi bila shuruti na inaendelea kuimarisha mazingira ya uzalishaji na utayari wa ufanyaji biashara ili kodi iongezeke kwenda kutekeleza miradi ya maendeleo,” alieleza.
KODI YA MAJENGO
Msigwa alisema, Julai mwaka huu TRA imeanza kukusanya kodi ya majengo kupitia mita za umeme ambapo kila nyumba za kawaida italipiwa sh. 1,000 kwa mwezi na kila sakafu ya nyumba ya ghorofa inalipiwa sh. 5,000 kwa mwezi.
Alieleza kuwa matarajio ya serikali ni kukusanya sh. bilioni 46.517 kwa mwaka huu wa fedha.
“Naomba kusisitiza kuwa lengo la kuanzisha utaratibu huu ni kupunguza changamoto kubwa iliyowakumba wananchi walioshindwa kulipa kodi ya nyumba na wakajikuta wanaangukia katika faini kubwa.
“Lakini pia ina rahisisha ukusanyaji wa mapato na kupunguza gharama kubwa za makusanyo ya mapato hayo,” alisisitiza.
MALIPO YA NDEGE MPYA
Kuhusu mpango wa ununuzi wa ndege mpya tano, Msigwa alisema serikali imekamilisha malipo ya awali na tayari wataalamu wameshachagua muonekano wa ndege hizo zinazotarajiwa kuwasili nchini mwaka 2023.
Kwa upande wa huduma alisema, Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) limesharejesha safari za kwenda India zinazoanza leo, kusafirisha mizigo kwenda China na hivi karibuni litazindua safari za kwenda Nairobi na Lubumbashi.
UJENZI WA SGR
Akizungumzia kuhusu ujenzi wa Reli ya Kisasa ya Mwendokasi (SGR), alisema ujenzi wa kipande cha Morogoro-Dar es Salaam umefikia asilimia 93 na Morogoro-Makutupora kimefikia asilimia 67.55.
Alisema mwisho wa Novemba mwaka huu, serikali itapokea injini mbili na mabehewa 12 ya treni ya majaribio katika njia mpya ya SGR huku mabehewa mengine yakitarajiwa kuwasili Juni 2022 na mengine 59 yatafika 2023.
“Pia, kuna treni za vichwa vya umeme 10 na mabehewa 80 ambazo treni hizo zitakuwa na vichwa mbele na nyuma. Lakini kwa sasa muda wowote Dar es Salaam na Morogoro itaungana na treni ya wakandarasi ambayo kwa sasa inatembea kati ya Ngerengere na Pugu, itaweza kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro,” alieleza.
Kwa upande wa ujenzi wa meli, alisema maandalizi ya ujenzi wa meli zingine nne na ukarabati wa meli tatu katika maziwa makuu na bahari yanaendelea baada ya kusainiwa kwa mikataba Juni mwaka huu ambapo miradi hiyo mipya itagharimu sh. bilioni 447.3.
MUSSA YUSUPH Na FRED ALFED, DODOMA



























