WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, amefunguka uimara wa Katiba kwamba, umeleta amani, kupendana, kushirikiana na kuwepo kwa kasi ya maendeleo nchini.
Amesema kutokana na hilo, hakuna umuhimu wa kuwepo kwa mchakato wa katiba mpya kwa sasa na vyama vya upinzani wanaitaka si kwa ajili ya wananchi, bali kwa malengo yao binafsi.
Aidha, amesema hakatai kuwa, katiba inaweza kuwa na upungufu kwa baadhi ya vipengele, hivyo vyama vya upinzani, vinapaswa kusema eneo lipi lifanyiwe mabadiliko kama lipo, siyo kutaka katiba nzima ibadilishwe wakati bado ina ubora wa hali ya juu na ndiyo imeleta maendeleo makubwa nchini.
Akizungumza na mamia ya wananchi wa Kijiji cha Makose na Chogola, Kata ya Masa, Jimboni kwake Kibakwe, Wilayani Mpwapwa, Mkoa wa Dodoma, jana, Waziri Simbachawene alisema sekeseke na
UKAGUZI
vurugu nyingi za vyama vya upinzani ni kuzungumzia katiba ambayo haina kosa lolote na shida kuu ya wananchi ni vitu vya maendeleo, siyo Katiba.
“Unakuta mtu anaisema katiba mbaya kwa kipengele kimoja tu cha Tume ya Uchaguzi, basi, lakini Katiba hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiyo iliyotuweka katika hali ya kupendana, nchi ya amani.
“Katiba hii ya Tanzania ndiyo inayopelekea Watanzania wanamiliki rasilimali na maliasili kwa umoja bila kuwa na ugomvi, nchi nyingine kila siku wanapigana mapanga kwa sababu rasilimali za nchi zao zimewekwa katika mazingira ambayo Katiba yake haijaweka vizuri na watu wanagombana kila kukicha,” alisema
Simbachawene aliongeza kuwa, katiba ya Tanzania ni nzuri, hakuna kitu ambacho hakikosi upungufu, hivyo kasoro za hapa na pale, zinaweza zikawa zipo na zinapaswa kushughulikiwa, siyo kuibomoa katiba yote, vinaweza vikachukuliwa vipengele muhimu vikarekebishwa kwa vile ambavyo vinavyopigiwa kelele.
“Shida ya Watanzania siyo katiba mpya, ila shida wanaotaka madaraka kwa njia nyepesi ndiyo, wanaona ni katiba, shida ya katiba ni ya watu wachache tu kwa malengo, kwa ubinafsi wao, lakini Tanzania hakuna shida ya katiba maana hii ni nzuri na imetupitisha katika vipindi muhimu na vigumu,” alisema
Waziri huyo aliyataja masuala mbalimbali ya maendeleo wanayoyataka jimboni humo ikiwemo maji, zahanati, barabara nzuri, shule kujengwa zaidi, nyumba za walimu na madaktari, lakini hawakusema wanataka katiba mpya, hivyo si shida ya wananchi zaidi ya kutaka maendeleo.
Aidha, aliwataka wananchi wa Kata ya Masa, kuhakikisha wanatunza mazingira kwa kutokata miti, kuharibu vyanzo vya maji na kusababisha barabara, mashamba, madaraja kuharibika kutokana na maporomoko ya maji kutoka milimani baada ya baadhi ya wananchi kuharibu mazingira hayo.
Simbachawene alimaliza ziara jimboni kwake kwa kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo na kutatua changamoto
NA MWANDISHI WETU, KIBAKWE



























