MAKAMU wa Rais Dk. Philip Mpango, ameagiza wakandarasi na wasimamizi wa ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), kuhakikisha ujenzi wake unazingatia utaalamu na vigezo.
Dk. Mpango aliyasema hayo, alipotembelea mradi huo katika maeneo manne ya ujenzi wa tuta kuu, njia ya kupeleka maji kwenye mitambo, sehemu itakayofungwa mitambo ya kuzalisha umeme na kituo cha kupokea na kusafirisha umeme.
Makamu wa Rais aliwasili katika mradi kwa kutumia usafiri wa treni ya TAZARA na kupokewa stesheni ya Fuga, ambapo alioona kazi mbalimbali za ujenzi katika maeneo hayo zikiendelea.
Alisema hitilafu itakayoonekana au kujitokeza katika mradi huo, ni vyema taratibu za kitaalamu zikatumika kuhakikisha ubora unazingatiwa ili usilete madhara.
“Huu mradi unajengwa na binadamu una uwezo wa kubomoka na kusababisha madhara makubwa, niwaombe kila mtakapoona kuna umuhimu wa kufanya marekebisho fanyeni hivyo kwani mrdi huu ni muhimu kwa taifa la Tanzania,”alisema Dk. Mpango.
Makamu wa Rais alisema Tanzania haiwezi kujenga uchumi wa viwanda bila kuwa na umeme wa uhakika wa kutosha utakaotoka katika bwawa hilo na ziada ya kuuza nje ya nchi.
“Dhamira ya Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha mradi huu unamalizika, Kasi hii inayoendelea nimeridhishwa na ujenzi wake na Mungu awarehemu viongozi wetu waliokuwa na ndoto juu ya mradi huu kwasababu ndoto zao zinatimia,”alisema.
Kuhusu mazingira, Dk. Mpango aliwataka wakuu wa wilaya na mikoa inayozunguka bonde la Rufiji kusimamia uhifadhi wa mazingira na kuhakikisha uchomaji wa moto haufanyiki.
Aliwataka wanasiasa wakiwemo wabunge kutoa elimu kupitia mikutano yao kwa wananchi kuhusu umuhimu na faida za utunzaji wa mazingira kwa kuwa Bwawa la Nyerere linategemea kupata maji kutoka katika vyanzo mbalimbali.
Awali, Dk Mpango alipokea taarifa inayohusu mradi huo kutoka kwa msimamizi wa mradi kutoka kitengo cha ushauri wa uhandisi wa Wakala wa Barabara Nchini (Tanroads), (TECU) Mhandisi mkazi John Mageni.
Waziri wa Nishati January Makamba alisema mradi huo ni muhimu, hivyo serikali inautazama kwa jicho la kipekee.
Na WARIOBA IGOMBE, RUFIJI



























