MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Philip Mangula, ameweka wazi jinsi chama hicho kinavyoziishi falsafa za Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Kesho, Baba wa Taifa anatimiza miaka 22 tangu afariki dunia katika Hospitali ya St. Thomas nchini Uingereza.
Kiongozi huyo amesema enzi za uhai wake, Hayati Nyerere aliamini katika umoja na haki, mambo yaliyojengwa na yanayoendelea kujengwa na uwepo wa vikao rasmi katika ngazi zote za uongozi.
Mangula alitoa kauli hiyo Dar es Salaam, wakati akihutubia mamia ya washiriki wa Kongamano la Kumbukizi ya miaka 22 ya Kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, lililofanyika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA).
“Mwalimu alijenga msingi wa kukutana ndani ya TANU, umoja unajengwa na vikao kwa sababu, mnaingia wajumbe wengi, kila mmoja ana mawazo yake, lakini mnatoka na wazo moja,” alisema Mangula.
Kadhalika alisema CCM kwa imani yake, kinaamini kwamba Binadamu wote ni sawa na kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake.
“Pia tunaamini kuwa, Ujamaa na Kujitegemea ndiyo njia pekee ya kujenga jamii ya watu walio sawa na huru,” alisema.
Makamu mwenyekiti huyo, alisema imani hiyo, imekuwa mwongozo wa yale aliyoyaamini Mwalimu Nyerere, ambaye alikuwa muumini wa umoja na mshikamano.
Alisema Mwalimu kwenye kitabu chake cha ‘Tumetoka Wapi, Tunakwenda wapi,’ amefafanua vizuri juu ya umuhimu wa umoja, kuelewana na kuwa ndugu.
“Sisi tunaamini kuwa, hakuna umoja bila haki, falsafa ambayo Mwalimu Nyerere, aliishi,” alisema.
Alisema katika kuhakikisha viongozi wanakuwa na maadili na kuzingatia haki na umoja katika utendaji wao, viongozi wa CCM walikuwa wakipewa mafunzo ya siasa na uongozi.
“Haikuwa rahisi mtu awe Mwenyekiti wa Chama Wilaya au Katibu wa Chama Wilaya bila kupitia mafunzo, lazima uwe umepita Kivukoni (chuoni),” alisema.
Kiongozi huyo alifafanua kuwa, katika kulidumisha hilo, CCM kwa kushirikiana na vyama vingine vya ukombozi kusini mwa Afrika, kimejenga chuo cha uongozi, Kibaha mkoani Pwani ili kuendelea kuwapika viongozi kimaadili.
Akizungumzia mada aliyopewa kuiwasilisha katika kongamano hilo, iliyohusu mchango wa Mwalimu Nyerere, katika kudumisha umoja, amani na maendeleo ya jamii, Mangula alisema Mwalimu aliweka misingi imara.
Aliitaja baadhi ya misingi hiyo kuwa ni kuanzishwa kwa Azimio la Arusha na Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, ambayo iligusa maisha ya jamii katika nyanja zote.
Na WILLIAM SHECHAMBO





























