WAZIRI wa Nishati, Januari Makamba, amesema kicheko au kejeli ya kuchelewa kwa mradi wa bwawa la kufua umeme wa maji la Julius Nyerere (JNHPP-MW2115) haimsaidii mtu.
Hayo ameyasema bungeni leo, Novemba 9, 2021 wakati akijibu hoja zilizotolewa na wabunge wakati wa mjadala wa mapendekezo ya mwongozo wa maandalizi ya mpango wa Bajeti ya Serikali na mapendekezo ya mpango wa maendeleo wa taifa kwa mwaka 2022/23.
Makamba amesema ni kweli mradi una changamoto za kawaida ambazo zipo kwenye utekelezaji wa Miradi mikubwa lakini haiwezi kuturudisha nyuma kama nchi.
“Tayari tumechukua hatua mbalimbali ambapo tumekaa na mkandarasi anayeutekeleza ili kumaliza changamoto hizo ya muda wa utekelezaji kuongezeka siku hizo zipungue badala ya kuwa 477 ziwe chache zaidi. Pia, kazi imalizike kwa wakati, kusiwepo ucheleweshwaji, wala gharama za ziada,”.amesema Makamba
Ameongeza :” Miradi yote itatekelezwa, kuchelewa kwa siku 477 haitaua mradi maana tumejipanga kuutekeleza lakini tarehe ya kujaza maji Kwenye bwawa imekaribia, ili kufanyika hilo kuna kazi zinatakiwa kufanyika ikiwemo kujenga ukuta na njia ya kuchepusha handaki lazima lizibwe kwa milango mikubwa na migumu 14 yenye tani 26 Kila mmoja,”.
“Hatutajaza maji kabla ya Machi mwakani kama ilivyopangwa awali, tutatoa tarehe rasmi, hivyo kicheko au kejeli ya kuchelewa kwa mradi haimsaidii mtu.” amesisitiza Makamba.
Na SELINA MATHEW, DODOMA



























