NGARIBA Mstaafu Hawa Njolo, kutoka mkoa wa Singida amewasihi wadau wa kupiga vita vitendo vya ukeketaji kwa watoto wa kike na ukatili wa kijinsia kutoridhia azimio la kutoa elimu kwa Vijana wakiume kutowaoa mabinti wa kike ambao tayari walishafanyiwa ukeketaji.
Ngariba Hawa ametoa rai hiyo jijini Dodoma wakati wa Uzinduzi wa mkakati wa Taifa wa kutokomeza ukeketaji nchini 2020/21-2024/25 na Uzinduzi wa Kikosi kazi Cha Kitaifa cha kusimamia na kuchakata masuala yote ya ukeketaji na kuhakikisha mkakati huo unafanikiwa.
Amesema mpaka sasa ndani ya jamii kuna idadi kubwa ya watoto wa kike ambao wameshawafanyia vitendo vya ukeketaji hivyo wakipitisha azimio hilo itakuwa ni kufanya ukatili juu ya ukatili kwa watoto hao.
Ngariba huyo amesema kwa kuwa makosa yalishafanyika, kinachopaswa kufanywa hivi sasa ni kupinga na kupambana na vitendo hivyo kwa kizazi cha sasa ili kisikeketwe.
Wakati wadau hao wakizindua mpango huo uku baadhi ya mangariba wakisalimisha silaha zao za ukeketeji kuashiria kuachana na vitendo hivyo, wapo baadhi ya mangariba wanaoendelea na kazi hiyo ambapo wamebuni mbinu mpya ya kukeketa watoto wakiwa wachanga ambayo ni hatari zaidi.
Na Happiness Mtweve, Dodoma





























