WAZIRI Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu, amewapiga marufuku Wakurugenzi wa Halmashauri kutoa adhabu ya kuwashusha vyeo walimu wakuu na maofisa elimu kata kwa kisingizio cha shule zao kutofanya vizuri.
Waziri Ummy ameyasema hayo katika Mahafali ya 29 ya Chuo cha Wakala wa Maendeleo ya Elimu (ADEM ) Bagamoyo mkoani Pwani kwa wahitimu wa stashahada ya uongozi na usimamizi wa elimu-DEMA, stashahada ya ukaguzi wa shule na astashahada ya uongozi, usimamizi na utawala katika elimu.
Amesema kabla ya kuwaadhibu na kuwashusha vyeo ni vyema kukafanywa tafiti za kina kujua sababu za taaluma mbaya katika shule hizo.
Aidha, amepiga marufuku watoto kusomeshwa muda wa ziada nyakati za usiku na kushindwa kupata muda wa kupumzika huku akiwaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya kusimamia shule za Sekondari za Serikali kuwapa likizo wanafunzi wote mwezi Desemba.
“Watoto wanapaswa wapumzike, haiwezekani mtoto kusoma shule na akirudi darasani usiku akeshe saa 2-9 alfajiri huko ni kumuumiza,
“Dakika 120 za kusoma zinamtosha, hapa niwaombe wazazi na walezi tusitake watoto wetu wahenyeshwe ndio tujue wanasoma sana ama shule ndio zinasomesha sana,” amesema Waziri Ummy
RUKSA KWA WALIMU
Amewaelekeza Wakurugenzi wa Halmashauri kutoa fursa kwa walimu kwenda kujiongezea elimu, “tumesomewa taarifa ya chuo kati ya walimu 1,345 walitakiwa kupokelewa kwenda kusoma walimu 408 hawakuripoti kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kukosa ruksa.
Aliongeza kwa kuhakikisha katika bajeti ya mwaka mpya wa fedha 2022/2023 Halmashauri zitatengewa fedha kwa ajili ya raslimali watu katika kuwaendeleza kielemu ili kuleta mabadiliko chanya katika elimu mashuleni.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu ADEM Dk. Siston Mgullah, alisema waliohitimu katika kozi fupi na ndefu katika masomo ya uongozi na usimamizi wa elimu , utawala na nyingine ni 1,082.
Alisema chuo hicho kinatarajiwa kuanzisha shahada ya kwanza ya menejimenti ya uthibiti ubora wa elimu kuanzia mwaka wa masomo 2022/2023.
Dk. Mgullah alifafanua kozi hiyo itavisaidia vyuo vya kati na vyuo vikuu kuwa na watumishi mahiri katika idara za uthibiti ubora wa mafunzo yanayotolewa.
Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo



















