WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, imedhamiria kulinda na kuimarisha afya za Watanzania, hasa wakati huu wa kutimiza dira ya kutokomeza UKIMWI nchini ifikapo mwaka 2030.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo, wakati akifungua Kongamano la Kisayansi la Kitaifa Kuhusu VVU na UKIMWI, katika Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani katika ukumbi wa Hoteli ya Mbeya Modern Highland , jijini Mbeya.
Amesema kaulimbiu ya kongamano hilo inayosema “Zingatia Usawa, Tokomeza Ukimwi, Tokomeza Magonjwa ya Mlipuko” inaakisi dhamira ya serikali ya kulinda na kuimarisha afya za Watanzania tunapoelekea kutimiza dira ya kutokomeza UKIMWI nchini ifikapo mwaka 2030.
“Hivyo basi nitoe rai kwa jamii kutafakari upya nafasi waliyonayo na kupinga kwa nguvu zote masuala yote na tabia zinazochangia maambukizi mapya ikiwemo unyanyapaa, ukatili wa kijinsia, mila zinazochangia maambukizi, ngono katika umri mdogo, kuporomoka kwa maadili na tabia nyinginezo hatarishi,”amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
Majaliwa ameeleza kaulimbiu hiyo imekuja wakati mwafaka ambapo taifa linahitaji kuihamasisha jamii na mtu mmoja mmoja kuzingatia usawa na kutoa mchango wake katika kufikia azma ya kutokomeza maambukizi mapya ya VVU hasa kwa vijana.
Vilevile, amesema serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya Mfuko wa Udhamini wa UKIMWI na kutafuta vyanzo vya uhakika vya kutunisha mfuko huo.
Waziri Mkuu amewashukuru wadau wa maendeleo kuendelea kufanya kazi na serikali katika utekelezaji wa miradi ya kudhibiti maambukizi mapya ya UKIMWI nchini.
Naye Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira na Wenye Ulemavu, Ummy Nderiananga, alisema wadau wote walioshiriki kongamano hilo, watumie ujuzi na maarifa waliyopata kuboresha kazi zao.
“Pia taasisi zinazojihusisha na masuala ya VVU na UKIMWI waongeze nguvu kwa kundi la wenye ulemavu,”alisema Ummy.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) Dk. Leonard Maboko alisema kongamano hilo ni fursa ya kutafakari walikotoka ili kuendelea kutekeleza afua za VVU na UKIMWI.
Alisema kongamano hilo linawapa fursa nzuri ya kupata takwimu zinazowasaidia kuboresha utendaji kazi, ambapo alitoa mfano mwaka 2016/2017 walifanya tafiti na kubaini wanaume wako nyuma katika upimaji.
Mwakilishi wa Mratibu Mkazi wa PEPFAR Tanzania, Dk. Hiltruda Temba, aliishukuru serikali kwa dhamira ya dhati ya kutokomeza VVU na UKIMWI nchini na kuendelea kutoa kipaumbele katika huduma muhimu za kinga na utekelezaji mzuri wa afua za UKIMWI.
Alisisitiza kuwa serikali ina dhamira ya dhati ya kufikia malengo ya kuwa na asilimia 95 ya watu wanaoishi na VVU hali inayosababisha kutambua hali zao za maambukizi na kupata tiba, ambapo asilimia 95 ya waliotumia dawa za ARV wamepunguza maambukizi.
NA MWANDISHI WETU





























