MAKAMU wa Rais, Dk. Philip Mpango, amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wakuu wa Kanisa la Baptist Tanzania wakiongozwa na Askofu Mkuu Anorld Manase Molel, na kuwataka waendelee kuombea viongozi wa serikali ili wawatumikie vema wananchi.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, Chamwino, Dodoma, Makamu wa Rais aliwashukuru viongozi na waumini wote wa kanisa hilo kwa kuendelea kuliombea taifa katika kudumisha amani, umoja na mshikamano.
Dk. Mpango alisema jamii yoyote yenye maadili mema na uzalendo inatokana na mchango mkubwa unaotolewa na viongozi wa dini.
Alisema Kanisa la Baptist Tanzania limekuwa na mchango mkubwa katika kushirikiana na serikali kutoa huduma za kijamii, zikiwemo za elimu na afya hivyo aliwaasa viongozi hao kuendelea kutoa huduma hizo, ikiwemo kufungua upya chuo kikuu walichokuwa wanakimiliki hapo awali cha Mount Meru.
Makamu wa Rais aliwasihi viongozi hao wa dini kuendelea kuwaombea viongozi wa serikali ili kutenda yalio mema na kumtanguliza Mungu katika utumishi wao.
Alisema kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi viongozi wa dini wanapaswa kuwaelimisha wananchi kutumia mvua zinazoendelea kunyesha kulima mazao ya muda mfupi, ili kujipatia mazao ya chakula na biashara.
Makamu wa Rais aliwahakikishia viongozi hao wa dini kwamba, serikali itaendelea kupokea ushauri na maoni yao kutoka katika taasisi za dini na kuahidi changamoto zote walizozitoa Kanisa la Baptist Tanzania serikali ya awamu ya sita itazifanyia kazi.
ASKOFU MKUU MANASE
Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Manase, aliishukuru serikali kwa kuendelea kutoa uhuru wa kuabudu kwa makanisa yote hapa nchini na kuahidi Kanisa la Baptist Tanzania, litaendelea kuliombea taifa ili amani na mshikamano viendelee kudumu.
Askofu Manase aliomba serikali kusimamia kikamilifu misamaha ya kodi inayotolewa kwa makanisa wakati wa kutoa huduma mbalimbali, zikiwemo za elimu na Afya.
Viongozi hao wa Kanisa la Baptist Tanzania waliomba serikali kupitia upya sheria za usajili wa jumuiya za kidini hapa nchini, ili kulinda misingi iliyowekwa.
Aidha, alisema katika kuliletea taifa maendeleo wanaunga mkono suala la Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika mwaka 2022 na kuiomba serikali kuongeza kasi katika utoaji elimu ya sensa hiyo, ili wananchi wote watambue umuhimu wake.
Katika hatua nyingine, viongozi hao wa dini wameiomba serikali kuweka mkazo katika masomo yanayowafanya wahitimu kujitegemea, yakiwemo masomo ya kilimo na biashara.
NA MWANDISHI WETU, DODOMA





























