MGANGA Mkuu wa Serikali Dk. Aifelo Sichwaele, amesema serikali imepanga kufunga mitambo 55 ya hewa ya Oksijeni, katika hospitali mbalimbali hapa nchini.
Kati ya mitambo hiyo, saba imeshafungwa na 12 imeshaingia nchini na iliyobaki ipo katika hatua za ununuzi, lengo ni kutoa huduma bora za kukabiliana na changamoto ya ugonjwa wa UVIKO- 19.
Aidha, alisema serikali imeongeza wigo wa upimaji wa UVIKO-19 nchini, kutoka maabara moja iliyokuwa inapima ugonjwa huo iliyopo Jijini Dar es Salaam katika maabara ya Taifa ya afya ya jamii na kuongeza vituo zaidi.
Dk.Sichwale alisema hayo Jijini Arusha wakati akizindua mpango harakishi na shirikishi awamu ya pili, wa uhamasishaji na utoaji wa chanjo ya UVIKO- 19, ulioshirikisha wadau mbalimbali wakiwemo waratibu wa afya ngazi ya mkoa kutoka mikoa yote 26, kutoka sekta za umma , binafsi na waandishi wa habari.
“Serikali tumejipanga kikamilifu kuimarisha upatikanaji wa hewa tiba ya Oksijeni nchini, ambapo tuna mpango wa kusimika mitambo 55 ya kuzalisha hewa hii katika hospitali mbalimbali. Kati ya mitambo hii saba imeshafungwa ,12 imeshaingia nchini kupitia fedha za serikali na iliyobaki ipo katika manunuzi,” alifafanua Mganga Mkuu wa Serikali.
WIGO WA UPIMAJI
Dk.Sichwale alisema serikali imeongeza wigo wa upimaji wa UVIKO-19, ikiwa ni pamoja na kufanya tafiti ili kubaini masuala mbalimbali, yakiwemo ya mitazamo ya jamii juu ya ugonjwa huo, afua za kukabiliana nao, tabia za ugonjwa huo na ushiriki wa jamii katika mapambano hayo.
Kuhusu juhudi nyingine za kukabiliana na ugonjwa huo, Dk.Sichwale, alisema serikali iliridhia matumizi ya chanjo ya UVIKO-19, ambapo mpaka sasa jumla ya dozi milioni 4.421.540 zimeshaingia nchini na kwamba, juhudi mbalimbali zinaendelea ili kupata chanjo zaidi kuchanja asilimia 60 ya wananchi .
“Tangu kuanza kwa zoezi hili nchini hadi Desemba 18 mwaka huu, jumla ya watu milioni 1,275,795 wamepata chanjo kamili dhidi ya UVIKO- 19, ambao ni sawa na asilimia 2.21 ya Watanzania wote”.
“Chanjo hii imetoa mwamko mkubwa kwa wananchi, bado tunaendelea kuhamasisha wananchi kuendelea kuchanja ili kujikinga na janga hili la UVIKO- 19,”alisema.
Kuhusu kuongeza wigo wa kupima ugonjwa wa UVIKO-19, alisema serikali imeongeza vituo vingine vitano ambavyo ni Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Arusha, Mbeya, Dodoma, maabara katika Hospitali ha Rufaa ya Bugando iliyopo Mkoa wa Mwanza na maabara katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, lengo likiwa ni kurahisha upimaji huo katika mikoa yote nchini.
“Ili kukabiiana na ugonjwa huu tunaendelea kuimarisha ufuatiliaji wa hali za ugonjwa na uchunguzi wa afya kwa wasafiri katika maeneo ya viwanja vya ndege nchini, bandari na mipaka ya nchi kavu, ili kubaini na kuzuia kuingia kwa maambukizi na anuai mpya za kirusi nchini,” alifafanua.
Aliongeza, “Pia tunaendelea kutoa huduma kwa wagonjwa wanaougua ugonjwa huu, huduma hii imeendelea kuimarika zaidi kwa serikali kuandaa miongozo mbalimbali na kutoa mafunzo endelevu kwa watumishi juu ya ugonjwa .”
Aidha, alisema serikali inaendelea kufuatilia rasilimali fedha za kukabiliana na ugonjwa huo, ambapo hivi karibuni kwa msukumo wa Rais Samia Suluhu Hassan, nchi ilipata mkopo wa shirika la Fedha la Kimataifa (IFM), wa kunusuru sekta zilizoathirika, ikiwemo ya afya ili kufufua uchumi.
NA LILIAN JOEL, Arusha





























