WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amekagua uimarishaji mpaka wa kimataifa baina ya Tanzania na Kenya, katika eneo la hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara na kuwapongeza wapimaji kuweka alama 205.
Aidha, Waziri Lukuvi aliwashukuru marais wa Tanzania na Kenya kukubaliana kuendelea na kazi ya uimarishaji mpaka huo wa kimataifa katika eneo la hifadhi ya Taifa ya Mbuga ya Serengeti na Masai Mara kwa upande wa Kenya, ambapo uimarishaji wake ulisimama kwa muda.
“Kwa muda mfupi timu za nchi hizo mbili zimeweza kuweka alama 205 katika eneo hili, kazi ilianza 2018 tulipofika eneo la hifadhi tulisiamama kidogo na uendelezaji unaofanyika umechangiwa na ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan kule nchini Kenya kuzungumza na mwenzake Uhuru Kenyata na kukubaliana na ndiyo maana wapimaji wamendelea na kazi hiyo,’’ alisema Lukuvi.
Akiwa katika eneo la Serengeti Desemba 21 2021 katika ziara ya kukagua uimarishaji mpaka wa kimataifa kati ya Tanzania na Kenya, Waziri Lukuvi alisema nchi hizo zitamaliza kuweka alama katika mpaka mzima unaofikia kilomita 758, ambapo kwa sasa zimefikiwa kilomita 232.
Kuhusu eneo la ukingo wa mpaka (Buffer Zone) Waziri Lukuvi alisema ni vyema utengenezaji barabara ukazingatia eneo la mita tano aliyoieleza kuwa ni mwafaka wa nchi hizo mbili na kuongeza kuwa, mazungumzo yanaendelea kuona kama kuna sababu ya eneo hilo kuongezwa.
‘’Serikali itaendelea kusaidia ili kazi hii ya uimarishaji mipaka ya kimataifa iende vizuri na uwekaji alama hizi siyo uadui bali ni kuwa na mipaka inayoonekana itakayoondoa hofu. Kama mtu akitaka kufanya uovu asisingizie kama hajui mpaka na alama tutaweka kote hata majini’’. Alisema Waziri Lukuvi.
Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Hamdouny Mansour alisema kazi mbalimbali zimefanyika wakati wa uimarishaji mpaka mpaka huo zikiwemo utoaji elimu, kuanisha sehemu ya kujenga, kujenga alama za mpaka pamoja na kukusanya taarifa za kijiografia.
Mpimaji kutoka Idara ya Upimaji nchini Kenya, Ibrayan Sabwa alisema katika kipindi chote cha kazi ya uimarishaji mpaka eneo la hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Masai Mara kwa upande wa Kenya, wamekuwa na ushirikiano mzuri baina ya timu za nchi hizo na kubainisha kuwa na hakukuwa na shida wakati wa kazi hiyo.
Mpaka wa Tanzania na Kenya una urefu wa nchi kavu wa kilomita 758 uliowekwa kwa makubaliano ya wakoloni wa Kijerumani na Kiingereza mwaka 1893 chini ya mkataba wa Anglo-Germany Agreement na Protocal kukubalika mwaka 1906.
NA MWANDISHI MAALUMU





























