RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amehimiza Vyuo Vikuu vya Zanzibar na taasisi za elimu ya juu, kuendelea kuanzisha programu mpya kwa utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya nchi na mahitaji yaliyoko katika soko la ajira.
Amesema vyuo hivyo lazima vishike usukani katika kukuza ubunifu na viwe tayari kushiriki kubuni mipango ya elimu na maendeleo kwa nchi.
Dk. Mwinyi aliyasema hayo katika hotuba yake iliyosomwa na Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla, katika mahafali ya 19 ya Chuo Kikuu cha Zanzibar, kilichoko Kibele, Mkoa wa Kusini Unguja.
Alisema jambo hilo sio jema ikizingatiwa Zanzibar ni kisiwa kilichozungukwa na bahari na tayari imetungwa dhamira ya kuifanya Zanzibar kuwa ni kitovu muhimu cha biashara na teknolojia ya bahari katika ukanda huu wa afrika mashariki.
Dk. Mwinyi alisema ni dhahiri kwamba ili kuweza kufikia lengo hilo basi vyuo vikuu ni lazima kuwa mstari wa mbele katika kutoa mafunzo na kufundisha programu mbali mbali zinazohusu fani hizo.
Hata hivyo alisema amefurahi kuona chuo hicho kimeanzisha programu mpya za masomo yanayohusu taaluma ya afya katika ngazi ya udhamili na udhamivu.
“Naupongeza sana uongozi wa chuo kuchukua uamuzi huo ambao unaenda sambamba na malengo ya serikali ya SMZ ya kuimarisha sekta ya afya kwa kuongeza idadi ya wataalamu, vifaa tiba na uimarishaji wa miundombinu,” alisema.
Alisema hospitali hizo zitajengwa kwa kutumia fedha za mkopo zilizoombwa kutoka shirika la fedha duniani kukabiliana na athari za kiuchumi na kijamii zinazotokana na janga la maradhi ya uviko 19.
Alisema lengo la serikali ni kuhakikishwa kila wilaya inakuwa na hospitali yake ya kisasa yenye kutoa huduma zote muhimu.
Aidha alitoa shukrani kwa vingozi wa taasisi binafsi za elimu katika ngazi mbalimbali kwa kuendelea kufanya kazi kwa karibu zaidi na serikali katika kukuza na kuimarisha ubora na viwango vya elimu inayotolewa Zanzibar.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Simai Mohammed Said alisema, wao kama Wizara ya Elimu wamepanga mambo makubwa katika kuleta mabadiliko katika sekta ya elimu ya juu.
Alisema watasomesha masomo katika vyuo vikuu hivyo ambayo yatawafanya wanafunzi kuweza kuitumia elimu hiyo katika nchi yake.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Zanzibar, Profesa Abdulkadir Othamn Hafidh alisema wahitimu 616 wamehitimu na kunutukiwa cheti, astashahada na shahada.
Kwa upande wao wanafunzi waliohitimu waliushukuru uongozi wa chuo hicho kwa juhudi mbalimbali walizofanya mpaka kufikia kuhitimu masomo yao.
Rukkayah Ali Othaman aliyehitimu ngazi ya astashada katika kozi ya utawala na biashara alisema, anakishukuru chuo hicho na ataitumia vizuri elimu yake aliyoipata.
Naye Simai Haji Mati alihitimu ngazi ya shahada alisema, hakuna mwisho wa kupata elimu na kwamba kila wakati jamii inatakiwa kujifunza kwani kila siku hutokea mambo mapya ambayo yanahitaji wataalamu.
NA HANIFA RAMADHANI, ZANZIBAR




























