RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameshuhudia utiaji saini wa miradi mikubwa ya uwekezaji baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Kampuni ya ‘Eagle Hills Regional Properties’ ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Kitengo cha Habari Ikulu Zanzibar, utiaji saini huo kwa upande wa Zanzibar ulifanywa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) Shariff Ali Shariff na Kampuni ya ‘Eagle Hills Regional Properties’ Mohammed Ali Rashid Alabar.
Awali, mwekezaji huyo alimweleza Rais Dk. Mwinyi kuridhishwa na mazingira ya uwekezaji Zanzibar, ambayo ni tofauti na alivyotembelea mataifa mengine duniani walikowekeza miradi mikubwa.
Alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais Dk. Mwinyi kumuunga mkono na kuahidi atafanya kila linalowezekana kuhakikisha uwekezaji anaotarajia kuufanya unafanikiwa.
MIRADI YA UWEKEZAJI
Miradi inayotarajiwa kujengwa na mwekezaji huyo ni hoteli ya nyota tano eneo la Kizingo, Mjini Zanzibar na nyumba kwa ajili ya maeneo ya makazi.
Eneo jingine litakalonufaika na uwekezaji huo ni Matemwe katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, ambako kutajengwa hoteli ya nyota tano na nyumba za kuishi zenye hadhi ya juu kwa ajili ya soko la watalii na watu wenye uwezo.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi alihudhuria sherehe za kuwatunuku vyeti washindi wa mpango endelevu wa Abu dhabi unaojikita kuendeleza masuala ya afya, chakula, nishati, maji na maendeleo ya elimu duniani zilizofanyika Dubai.
Rais Dk. Mwinyi katika shughuli nyingine aliyoifanya ni kutembelea banda la Tanzania katika maonyesho ya Kimataifa ya Dubai yanayojulikana kama ‘Expo 2020’.
Rais Dk. Mwinyi anaendelea na ziara katika nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), inayotarajiwa kumalizika leo na baadaye kurejea nyumbani.
NA MWANDISHI MAALUMU, ABU DHABI




























