MAKAMISHNA wa ardhi wasaidizi wa mikoa wametakiwa kuhakikisha wanawawekea vipimo vya utendaji kazi watumishi wa sekta hiyo, kila baada ya mwezi mmoja.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Mkazi, Ridhiwan Kikwete, alitoa agizo hilo jijini Dar es Salaam, alipozungumza na watendaji wa sekta ya ardhi wa mkoa huo na baadhi ya watumishi wa sekta hiyo mkoa wa Pwani katika ziara yake baada ya kuteuliwa hivi karibuni.
Aliwataka wataalamu wa sekta ya ardhi kuwa wabunifu sambamba na kutoa huduma bora na kwa wakati ili kuisaidia serikali na wananchi kwa ujumla.
“Makamishna wangu haya sasa ni maagizo, hao maofisa wenu wote katika idara zenu zote wawekeeni vipimo vya kupima utendaji kila baada ya mwezi mmoja ili kujua nani anafanya kazi na nani hafanyi kazi. Kujua idara gani inafanya kazi na idara gani haifanyi kazi,’’ alisema.
Aliongeza kuwa kama watendaji wa sekta ya ardhi wataendelea kufanya kazi kwa mazoea na kuzalisha migogoro kila siku basi sekta ya ardhi haitapiga hatua.
Alieleza baaadhi ya watendaji ni mafundi wa kuzalisha migogoro na baadaye hupita mlango wa nyuma kwenda kuimaliza jambo alilolieleza hayuko tayari kuvumilia tabia hiyo kwa kuwa upo Mfumo Unganishi wa Taarifa za Ardhi (ILMIS) unaoweza kuzitafutia ufumbuzi baadhi ya changamoto za ardhi.
“Mfumo wetu wa ILMIS uko vizuri na umeanza mkoa wa Dar es Salamaa, tunataka kuupeleka mikoa mikubwa na baadaye nchi nzima maana tufikie mahalali majawabu ya shida zetu kuyapata kupitia mfumo,” alisema.
Alisisitiza kuwa hatakuwa tayari kusikia Rais Samia Suluhu Hassan anabebeshwa lawama asizostahili kuhusiana sekta ya ardhi na kuweka bayana kuwa, kama yupo mtu anayedhani anaweza kufanya jambo la hovyo ajue utaratibu huo umekwisha.
Aliwataka wataalamu wa sekta ya ardhi kuwa wabunifu sambamba na kutoa huduma bora na kwa wakati na kuacha kufanya kazi kwa mazoea ili kuisaidia serikali na wananchi kwa ujumla.
“Nawaomba muwe wabunifu na muache kufanya kama kazi yako, ni ofisa ardhi usipoletewa vifaa eti unalala, hiyo haiwezekani na kama hakuna vifaa waombe wakubwa zako ili wao waone sababu ya kupeleka vifaa ili upime ardhi kwa kuwa ardhi ni uchumi,’’ alisema.
NA MWANDISHI WETU



















