SERIKALI imetenga kiasi cha sh. bilioni 1.38 kupitia fedha za Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Mapambano dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya hospitali na ununuzi wa vifaa ili kuboresha huduma za afya wilayani Sikonge Mkoani Tabora.
Akizungumza na UHURU, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Seleman Pandawe amesema serikali imetenga kiasi hicho cha fedha ili kuwaondolea kero ya upatikanaji huduma bora za afya wananchi wa wilaya hiyo.
Amesema fedha hizo zimelenga kuboresha huduma za afya ya msingi katika hospitali mpya ya wilaya hiyo ikiwemo ujenzi wa jengo la dharura (EMD), ujenzi wa nyumba za watumishi (3 in 1), ununuzi wa vifaa vya huduma za dharura (EMD) na ununuzi wa mashine ya x-ray.
Amebainisha kuwa tayari wamepokea kiasi cha sh. milioni 390 ambapo sh. milioni 300 zitatumika katika ujenzi wa jengo la dharura na sh. milioni 90 katika ujenzi wa nyumba za watumishi.
Mkurugenzi alifafanua kuwa ujenzi wa majengo hayo utatumia mfumo wa ‘force account’ na kwa sasa wapo katika hatua ya manunuzi na mchakato utakapokamilika utapunguza kiasi kikubwa vifo na kuboresha huduma za matibabu wilayani humo.
“Tunamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia fedha hizo, zitasaidia sana kuboresha huduma za afya kwa wananchi wetu’, alisema.
Pia, aliomba serikali kuendelea kutenga fedha zaidi na kuwapatia ili kuharakisha utekelezaji miradi ya afya ikiwemo ujenzi wa zahanati katika kila kijiji na vituo vya afya katika kila kata ili kupunguza adha wanazopata wananchi.
Naye, Mganga Mkuu wa wilaya hiyo (DMO), Dk. Theopister Elisa, amesema, mbali na ujenzi wa jengo hilo serikali itawaletea vifaa vyenye thamani ya sh. milioni 371 na mashine ya x-ray yenye thamani ya sh. milioni 420.
Hivyo, alisema kukamilika kwa miradi hiyo, ikiwemo vifaa vya kutolea huduma kutaboresha kwa kiasi kikubwa huduma za afya ya jamii wilayani humo na kupunguza malalamiko ya wananchi.
Na Allan Kitwe, Sikonge



























