RAIS Samia Suluhu Hassan,ametoa maagizo zaidi ya saba likiwemo la kuwataka wakuu wa mikoa nchini kutekeleza operesheni maalum ya anwani za makazi kwenye maeneo yao kwa kushirikisha wananchi, ili mfumo huo ukamilike kabla ya Mei, mwaka huu kwa kuwa ndio kipimo cha utendaji wao.
Aidha, ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango kukabidhi haraka kiasi cha sh. bilioni 28 kwa wakuu hao wa mikoa, ili zigawanywe kama za Uviko-19 kwa ajili ya utekelezaji wa mfumo huo pande zote mbili.
Rais alitoa maagizo hayo jijini Dodoma, Februari 8, 2022, wakati wa kikao kazi cha kukabidhi mfumo wa anwani za makazi kwa wakuu wa mikoa kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa, ambapo alitaka fedha zake kutumika kama ilivyokuwa za mradi wa Uviko-19.
“Wakuu wa mikoa; awali baada ya tathmini kufanyika niliambiwa mradi utatumia sh. bilioni 700 nikajiuliza mbona fedha nyingi, lakini baada ya kutumia wataalamu wa mamlaka za Serikali za Mitaa imeshuka mpaka sh. bilioni 28, hivyo tutaleta kwenu hizo fedha tugawane kwa ukumbwa wa mkoa pande zote mbili, tambueni sio OC (matumizi mengine), ni za miradi,”aliagiza Rais Samia.
Aliongeza kuwa: “Wizara ya Fedha zigaweni fedha hizo kama ulivyokuwa mgawo wa fedha za mradi wa Uviko-19 kwa ukubwa wa mkoa, kwa maana hiyo Bara na Zanzibar mtapata kiwango tofauti, zishaurini halmashauri zichange fedha maana kuna fedha zinaliwa huko.”
“Ni lazima tutumie nyenzo zilizopo kukamilisha zoezi hilo, kama kuna wananchi wanataka urembo kwenye maeneo yao wafanye hivyo kwa gharama zao, Serikali hatuhusiki,”alisema na kuziagiza wizara za kisekta kuhakikisha zinampa taarifa za utekelezaji mara kwa mara kuhusu maendeleo ya zoezi hilo ili kama kuna changamoto zifanyiwe kazi.
Rais samia aliongeza kuwa: “Kazi ifanyike kama operesheni maalum kwa muda uliopangwa na hakikisheni mnashirikisha wananchi, ili ifikapo Mei RC ambaye atakuwa hajamaliza itabidi kukutana ana kwa ana tuelezane na kama una changamoto sema mapema tuzitatue.”
Maagizo mengine, alizitaka taasisi mbalimbali zikiwemo TANROADS, TARURA kuzingatia sheria ya uwekaji majina kwenye barabara na kutoa ushirikiano kwa wakuu wa mikoa ili kufanikisha kukamilika kwa zoezi hilo.
Vilevile, Rais Samia aliagiza Wakala wa Majengo Tanzania(TBA),Shirika la Taifa la Nyumba (NHC) na Watumishi Housing kuhakikisha wakati wa utekelezaji wa miradi yao ziwepo anwani za makazi na watoe ushirikiano kwa wakuu wa mikoa ambao ni wasimamizi wakuu kwenye maeneo yao.
Aidha, Rais Samia aliwataka wabunge, madiwani kuwa mabalozi na kichocheo cha utekelezaji wa mfumo ili ukamilike kwa muda uliopangwa kwa kuwa ndio kigezo cha utendaji kazi wao.

WAKANDARASI
Wakati huohuo, Rais Samia alisema hawatatumika wakandarasi ambao walijiandaa kwa ajili ya kutekeleza zoezi hilo na badala yake kazi itafanywa na kamati za mikoa zenye uwezo.
“Najua mikoani wameandaliwa wakandarasi wanasubiri fedha zile sh. bilioni 700 kwa ajili ya utekelezaji, hivyo tumeachana nao na badala yake tutafanya wenyewe kuanzia ngazi za mikoa hadi chini undeni kamati zenye uwezo na ari ya kufanya kazi,”alisema.
Rais Samia alisisitiza kuwa kukamilika kwa mfumo huo kutawezesha kuibuka kwa mambo mengi yakiwemo ya Watanzania kuhifadhi kumbukumbu zao kwenye kituo cha utunzaji kumbukumbu na kila mmoja kuwa na anwani yake ya makazi.
“Nchi itang’ara kimataifa maana hadi leo tunaonekana washamba, tukienda nchi za wenzetu kwenye fomu unakuta umeambiwa ujaze anwani za makazi, lakini kwa sasa tunaenda kuvua ushamba maana ukikamilika ni muhimu kwa maendeleo ya nchi na sensa ya watu na makazi,”alisisitiza Rais.
MAKAMU WA RAIS
Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango aliwataka viongozi kueleza matumizi ya mfumo wa anwani za makazi kwa maslahi ya pande mbili za Muungano.
“Natambua moja ya kazi yako ni kuongoza mabadiliko ya haraka ya uchumi na maendeleo ya nchi, ukiwemo mfumo huo muhimu kwa maendeleo ya watu maana binadamu wana mfumo wa utawala hivyo ni nyenzo muhimu,”alisema Dk. Mpango.
WAZIRI MKUU
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema mchakato wa kupitia bajeti unaendelea ili fedha zitumike zilivyopangwa na kwa gharama nafuu ndio maana wameamua kupeleka zoezi hilo kwa mamlaka za serikali za mitaa, ili Watanzania washiriki kikamilifu.
MAKAMU WA RAIS SMZ
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, alibainisha kuwa anwani za makazi zikikamilika nchi itakuwa na historia maana halikuwa jambo rahisi ni la maendeleo hivyo kuahidi ushirikiano.
“Zoezi hili likisimamiwa vyema litaakisi lile lengo ambalo serikali inalitarajia, naamini wakuu wa mikoa wakisimamia litafanyika kwa ufanisi kuelekea kwenye zoezi la sensa, Zanzibar tunawahakikishia tupo imara na tayari kuwezesha ukamilishaji wake,”alisema.
WAZIRI NAPE
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, alisema utekelezaji wa mfumo huo ulitakiwa kutumia kiasi cha sh. bilioni 700 hadi kukamilika, lakini baada ya mpango kubadilishwa unatumia sh. bilioni 28 hivyo kuokoa kiasi cha sh. bilioni 668.
“Katika uongozi wa Rais Samia aliyofanya yanathibitsiha umahiri, uzalendo na mapenzi kwa Watanzania, ambapo hadi sasa mkongo wa taifa umekamilika kwa asilimia 55, anwani za makazi ilipangwa kufikia 2025 kata 4,067 ziwe zimefikiwa na mfumo, lakini zimefikiwa chache hivyo kasi kuonekena kwenda taratibu,”alisema Nape.
WAZIRI PINDI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dk. Pindi Chana, alisema ofisi hiyo imekuwa ikisisitiza taasisi zote kuweka miundombinu ya mfumo wa anwani za makazi katika maeneo ya wananchi kwakuwa ni suala mtambuka.
WAZIRI BASHUNGWA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Innocent Bashungwa, alisema ofisi hiyo itaendelea kuratibu ngazi za mkoa na mamlaka za serikali za mitaa kwa kutoa elimu kwa viongozi, watendaji na wananchi kuhusu mfumo huo.
WAZIRI RAHMA
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Rahma Kassim Ali, alisema wanaendelea na utekelezaji wa mfumo huo kwa ushirikiano wa karibu ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.
“Tayari tumechukua hatua ikiwemo kuandaa ramani za kidigitali, kufanya utambuzi wa barabara na mafunzo ya nadharia na vitendo yametolewa na baadhi ya kata (shehia),zimeshapewa majina ya mitaa,tutahakikisha mfumo unakamilika kwa wakati,”alisema Rahma.
N/W RIDHIWANI
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete, alisema kwa sasa wanaandaa ramani za kidigitali zitakazotumika kwenye mfumo huu ili kurahisisha upatikanaji taarifa sahihi za ardhi.
“Tunafahamu inatakiwa kukamilika kabla ya Mei hivyo tunaendelea kubadili ramani kutoka mfumo wa analojia kwenda kidigitali na upangaji ramani za mipango miji, ambapo zoezi limekamilika baadhi ya maeneo, tumejipanga kukamilisha kwa muda maana tutanufaika na taarifa hivyo kuimarisha ukusanyaji mapato kwa mfumo wa anwani za makazi,”alisema.
MAMA MAKINDA
Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi, Spika mstaafu Anne Makinda,alisema sensa ya mwaka huu itakuwa ya kipekee kuliko ya miaka iliyopita kwa kuwa itaendana na anwani za makazi.
“Tunamalizia kazi ya kugawa maeneo kwa ajili ya kuhesabiwa watu kupitia wenyeviti wa mitaa na vitongoji na sensa itafanyika kikamilifu kwake, lazima iendane na anwani za makazi na itakuwa the best kuliko zote zilizopita,”alisema mama Makinda.
RC MONGELLA
Mwenyekiti wa Wakuu wa Mikoa ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella, aliahidi kuwa watasimamia utekelezaji wa zoezi hilo kwa ufanisi wa hali ya juu.
RC MTAKA
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka, alisema kupitia utekelezaji wa mfumo huo wa anwani za makazi Mkoa wa Dodona utakuwa wa kipekee kati ya yote.
NA SELINA MATHEW, DODOMA



























