SERIKALI imesema haina sababu ya kuongeza maduka binafsi ya dawa, kwa kuwa yale yanayoimiliki yana uwezo wa kutosha wa kutoa huduma na kinachofanyika ni kuyaboresha ili zipatikane kwa wakati.
Hayo yalielezwa Bungeni, jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dk. Festo Dugange, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Msalala, Kassim Iddi (CCM).
Katika swali lake, mbunge huyo alitaka kujua serikali ina mpango gani wa kuwaunganisha na maduka ya dawa kwa kuwa kumekuwa na changamoto ya watu wa bima ya afya wanapokwenda zahanati au kituo cha afya kukosa dawa.
Dk. Dugange alibainisha kuwa suala hilo wanalifanyia kazi na walishatoa maelekezo katika mikoa yote ili kuongeza washitiri zaidi ya wawili na si kuwa na washitiri kila wilaya ambapo haitakuwa na tija.
Awali, katika swali la msingi mbunge huyo alitaka kujua ni lini serikali itatoa vifaa tiba na dawa za kutosha katika vituo vya afya na zahanati zote katika Halmashauri ya Wilaya ya Msalala.
Naibu waziri huyo alisema serikali imeendelea kutenga fedha kwa ununuzi wa vifaa tiba na dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
“Katika mwaka wa fedha 2021/22, serikali ilitenga shilingi bilioni 11.3 za ununuzi wa vifaa na vifaa tiba ambapo Halmashauri ya Msalala imetengewa shilingi milioni 376 kati ya fedha hizo,” alisema.
Alisema Halmashauri ya Wilaya ya Msalala katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022, imetenga bajeti ya dawa na vifaa tiba sh. bilioni 1.05 ambapo hadi kufikia Desemba, mwaka jana sh. milioni 178 zimetolewa.
Aliongeza kuwa Kituo cha Afya Isaka na Mwalugulu vimetengewa vifaa vya sh. milioni 600 na Zahanati ya Matinje, Mwakima na Kabondo zimetengewa sh.milioni 150 kwa vifaa na vifaa tiba. “Serikali itaendelea kuongeza fedha za dawa na vifaa tiba kadri ya bajeti itakavyoruhusu.
“Aidha, serikali imeshazielekeza mamlaka za serikali za mitaa kuimarisha usimamizi na udhibiti wa makusanyo ya fedha za mapato ya ndani ili kuhakikisha dawa na vifaa tiba vinapatikana katika utoshelevu na kutoa huduma bora kwa wananchi,”alisema.
Na Happiness Mtweve,Dodoma



















