CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimempongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuridhia ongezeko la mishahara na kupandishwa kwa malipo ya mkupuo ya pensheni kwa wastaafu.
Uamuzi wa kupandisha mishahara ikiwa ni pamoja na kima cha chini kwa watumishi wa umma kwa asilimia 23.3, ambao umefanyika kwa kuzingatia taratibu za mwenendo wa uchumi, pia ule wa kuelekeza kukamilishwa kwa taratibu za kisheria kuhakikisha malipo ya mkupuo ya wastaafu yanapandishwa kutoka asilimia 25 hadi asilimia 33.
CCM imetoa pongezi hizo ikiwa ni siku moja, baada ya Rais Samia kuridhia mapendekezo ya nyongeza ya kima cha chini kwa watumishi wa umma kwa asilimia 23.3, hatua ambayo inatekeleza ahadi yake aliyoitoa Mei mosi, mwaka huu katika sherehe ya Siku ya Wafanyakazi.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na kutiwa saini na Katibu wa Halmashauri Kuu Taifa, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, ilisema huo ni mwendelezo wa hatua kadhaa zinazoendelea kuchukuliwa na serikali ya CCM awamu ya sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kuboresha maslahi na stahiki za wafanyakazi nchini.
Ilisema tayari serikali ilishapunguza kodi ya mapato katika mishahara ya wafanyakazi (PAYE) kutoka asilimia 9 hadi 8, kufuta tozo ya kulinda thamani ya mkopo ya asilimia sita kwa wanufaika wa mikopo elimu ya juu wakati wa marejesho na upandishwaji wa madaraja kwa kuzingatia miundo ya utumishi wa kada mbalimbali.
“Hatua zote hizi ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 -2025, ibara ya 130, ukurasa wa 180-181. Aidha nyongeza ya mishahara ni utekelezaji wa ahadi ambayo Rais Samia Suluhu Hassan aliitoa kwa wafanyakazi kupitia hotuba yake kwa taifa Siku ya Wafanyakazi Duniani kuwa Jambo lao lipo na linafanyiwa kazi,” alisema.
Taarifa hiyo ilisema utekelezaji wake umedhihirisha jinsi Rais Samia alivyo kiongozi msikivu, anayejali wananchi wake, muungwana wa vitendo na zaidi yuko imara kuhakikisha Serikali ya CCM anayoiongoza, inaendelea kuwa tumaini la watu kwa kugusa maisha yao kwa namna chanya.
Pia, uamuzi wa nyongeza ya mishahara na malipo ya mafao kwa mkupuo umefikiwa baada ya kuwepo majadiliano yaliyohusisha serikali na wadau wanaohusika vikiwemo vyama vya wafanyakazi kupitia Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE).
“Mchakato huu umeendelea kuithibitishia dunia kwamba uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ni shirikishi na wenye uwazi sifa ambazo ndio msingi wa utawala bora,” ilisema.
Chama kinatoa wito kwa wafanyakazi nchini kuendelea kuiunga mkono serikali, kushikamana, kufanya kazi kwa bidii, uzalendo na weledi ili kuleta tija zaidi katika maendeleo ya nchi.
WACHUMI, WASOMI, WAFANYAKAZI WANENA
Wachumi, wasomi, wafanyakazi na wananchi wa kawaida, walisema ongezeko hilo la mshahara wa asilimia 23.3 inakwenda kuinua uchumi wa nchi na kwa mwananchi mmoja mmoja.
Walisema nyongeza hiyo inakwenda kuinua kipato cha mfanyakazi na mwananchi wa kawaida hususan mfanyabiashara mdogo, ambaye pato lake linakwenda kuongezeka.
Akizungumza na UHURU, Mkuu wa Idara wa Uchumi wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Dk.Timoth Lyanga, alisema, ongezeko la mshahara wa asilimia 23.3 unakwenda kuinua hali ya maisha ya mfanyakazi wa kima cha chini.
Dk. Lyanga alisema licha ya mfanyakazi wa kima cha chini anakwenda kupata manufaa katika mshahara huo, pia mwananchi wa kawaida naye anakwenda kufaidika na nyongoza iliyotolewa na Rais Samia.
“Kutokana na nyongeza hiyo mfanyakazi anakwenda kupata ziada ya mshahara wake, ambao ataufanyia mambo mengine ya kimaendeleo.
Alisema kutokana na nyongeza hiyo ya mshahara mfanyabiashara mdogo anakwenda kufaidika kwa sababu kama mfanyakazi alikuwa ananunua machungwa matano, lakini sasa atanunua machungwa 10.
“Hii nyongeza ya mshahara iliyotolewa na Rais Samia ina faida katika pande zote, hivyo inatakiwa kuendelea kumuunga mkono ili jitihada zaidi ziendelee kufanyika,” alisema.
Dk.Lyanga alisema nyongeza hiyo inakwenda kumuinua mfanyakazi kwa namna mbalimbali, ikiwemo hata kwenye suala la mikopo ya benki.
“Mfanyakazi aliyekuwa akikopa mshahara wa sh.milioni tano hivi sasa anaweza kukopa hadi sh.milioni saba, sasa hapo ndipo uchumi wa mtu unapoongezeka kwa sababu fedha hiyo anakwenda kuifanyia maendeleo ya kiuchumi, ikiwemo kuanzisha miradi mbalimbali ya uzalishaji mali na watu wengine kupata ajira,” alisema.
Hata hivyo, aliiomba serikali iendelee kuwadhibiti wafanyabiashara katika upandishaji wa bidhaa.
“Kwenye hili wafanyabiashara wasione ni fursa ya kupandisha bei ya bidhaa zao kiholela,” alisema.
Naye, msomi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk.Sylvester Rugeihyamu, alisema Rais Samia ametimiza kauli yake ya kusema kuwa anawajali wafanyakazi na Wwatanzania kwa ujumla.
Dk. Rugeihyamu alisema nyongeza ya mshahara huo utawafanya wafanyakazi wafanye kazi kwa bidii kwa ajili ya kuleta maendeleo nchini.
“Ni vizuri Rais Samia ameongeza nyongeza hiyo ya mshahara kwa sababu atakuwa ametoa joto kali walilokuwa nalo wafanyakazi kwa kipindi kirefu,” alisema Dk. Rugeihyamu.
Alisema nyongeza hiyo ya mshahara inakwenda kuondoa gharama za maisha alizokuwa anapata mfanyakazi wa kima cha chini.
Mwalimu Fausta Nyako, alisema Rais amefuta kilio chao cha muda mrefu.
“Rais amefuta kilio chetu cha muda mrefu, lakini na sisi tunatakiwa tushirikianae naye katika kufanya kazi kwa bidii ili uchumi wa nchi uzidi kuongezeka,” alisema Fausta.
Mwajuma Shabani ni mwananchi wa kawaida anasema nyongeza hiyo ya mshahara haifaidishi mfanyakazi peke yake hata yeye mjasiriamali anafaidika.
“Na sisi wajasiriamali tumefaidika na nyongeza aliyoitoa Mama kwa sababu wateja wataongezeka katika biashara yangu,” alisema.
Katibu wa Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania, Sheikh Mohamed Iddi, alimpongeza Rais Samia kwa kupandisha mishahara ya kima cha china kwa waumishi wa umma kwa nyongeza ya asilimi 23.3 na kupunguza baadhi ya kodi za makato kwa wafanyakazi.
Alisema Rais Samia ametekeleza ahadi hiyo aliyoitoa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani Mei mosi, mwaka huu kwa utaalamu mkubwa, kwani halikufanyika kwa kipindi cha miaka sita.
Iddi alisema Rais Samia ameshughulikia kikamilifu upandaji wa bei ya mafuta, kuunda kamati ya kutatua changamoto za kisiasa, kutangaza utalii.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi(UWT) Mkoa wa Njombe, Scolastika Kevela, amempongeza Rais Samia kwa kupandisha mishahara ya wafanyakazi nchini na hivyo kumaliza kilio chao cha muda mrefu.
Scolastika ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Udalali ya Yono Auction Mart, alisema hatua hiyo ya Rais Samia ni utekelezaji wa ahadi aliyokuwa ameitoa wakati wa maadhimisho ya siku ya wafanyakazi Duniani, ambapo pamoja na mambo mengine, aliahidi kuongeza kima cha mishahara kwa wafanyakazi jambo ambalo lilikuwa kilio chao kwa muda mrefu.
“Rais Samia Suluhu Hassan kwa hili anastahili pongezi nyingi sana, amedhihirisha wazi wazi yeye ni mama mwenye malezi mazuri na ujali kwa wanawe, madai ya nyongeza ya mishahara ilikuwa kilio cha miaka mingi nchini, kwetu sisi UWT Mkoa wa Njombe tunasema hana baya,” alisema.
Na WAANDISHI WETU



























