WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima, ameagiza Polisi Mkoa wa Arusha, kumsaka Mkazi wa Uswahilini jijini humo, Ally Abdallah, ambaye anadaiwa kumbaka mtoto wake wa kike mwenye umri wa miaka minne (jina linahifadhiwa) na kumharibu sehemu za siri.
Akizungumza jijini Arush katika ofisi za polisi mkoa, Dk. Dorothy alisema amefika mkoani hapo baada ya kupata taarifa kuhusu unyama aliotendewa mtoto huyo.
“Nimepata taarifa za kushtua na kusikitisha kuhusu mtoto wa miaka mine, aliyebakwa ambaye mama yake mzazi alitoa taarifa Kituo Kidogo cha Polisi Unga Ltd, lakini baadhi ya watu wakashauri amwachie Mungu. Hii haikubaliki, naagiza Kamanda wa polisi mkoa, ahakikishe mtuhuhumiwa wa tukio hilo atafutwe popote alipo na afikishwe mbele vya vyombo vya sheria.
“Nimeamua kwenda kumtembelea huyu mama eneo la Uswahilini jijini Arusha kuzungumza naye kwa kina, analia sana kwa sababu tukio hili limemwathiri kisaikolojia. Nimewaagiza wataalamu dawati la jinsia na maendeleo ya jamii wakae naye wampatie ushauri nasaha ili arejee katika hali ya kawaida,” alisema.
Waziri Dorothy alimhakikishia mama huyo kwamba wizara itasimama kidete kuhakikisha haki inatendeka na mtoto huyo kurejeshwa kwa mama yake mzazi.
Awali, akizungumza kwa uchungu mama wa mtoto huyo, Amina Abdallah (25), alidai alibakwa siku ya Sikukuu ya Eid el Fitri.
Alidai mtoto wake alikwenda kucheza na wenzake jirani na nyumba yao, baada ya muda alirudi akiwa na pipi mkononi huku akitokwa damu sehemu za siri.
“Baada ya kumuona mtoto wangu katika hali hiyo nilimwuliza kafanya nini akanijibu ameumizwa na kijiti. Nikamtishia nikamwambia usiponiambia ukweli nitajichoma kisu nife, lakini bado mtoto akazidi kusema amechomwa na kijiti,” alidai.
Amina alidai kutokana na majibu hayo alilazimika kumpeleka mwanae kwa majirani ili wamsaidie kumwuliza amepatwa na kitu gani, hakusema chochote na ndipo wakaamua kumchapa na kidogo alitoa maji mazito meupe sehemu za siri.
“Baada ya kuona maji hayo tulimkagua mtoto ndipo tukabaini kuwa amebakwa na kuharibiwa vibaya, hali iliyotulazimu mimi, mama yangu na majirani kwenda kituo kidogo cha Polisi Unga Ltd na kupewa fomu namba tatu kisha kumpeleka Hosptali ya Rufaa ya Mt. Meru kwa ajili ya matibabu,” alidai.
NA LILIAN JOEL, Arusha





























