KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, amesema uamuzi wa serikali kuwapanga vyema wafanyabiashara wadogo hauna lengo la kuwatia umasikini bali kuwajengea mazingira mazuri ya kujiongezea kipato.
Amesema kutokana na hilo ni vyema viongozi hususan wa halmashauri za wilaya kuhakikisha hawapindishi lengo hilo kwa kuwawekea wamachinga mazingira magumu ya kufanyia biashara.
Shaka ameyasema hayo mjini Babati, wakati akizungumza na wajasiriamali wadogo wanaofanya shughuli zao katika stendi ya zamani mjini Babati, mkoa wa Manyara ambao walilalamikia uamuzi wa kuwahamisha katika eneo hilo, huku wakisema walikopelekwa kuna mazingira magumu ya biashara.
“Uamuzi wa Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwapanga wamachinga katika maeneo rasmi hauna maana ya kuwatengenezea umasikini, bali kuwawekea mazingira mazuri ya kufanya biashara na kuwaongezea kipato,” amesema.
Shaka alitoa kauli hiyo baada ya kinamama wanaofanya biashara ndogondogo, ikiwemo ya nyanya katika eneo hilo kulalamikia changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo ikiwemo ya kusumbuliwa na mgambo wa Halmashauri.
“Mimi nimewaelewa na niwashukuru kwa maoni yenu na hiki ni Chama cha watu na kama chama cha watu lazima tuwasikilize wananchi, lakini kwenye hilo la kusikiliza ndio maana tumefuatana na wenzetu wa serikali ambao wanatoa ufafanuzi.
“Pale ambapo ushauri unahitajika, sisi kama Chama tunao uwezo wa kushauri, mimi niishauri serikali pamoja na kwamba, naamini dhamira ya Rais Samia ni njema sana na sisi Chama tunamuunga mkono kwenye jambo hili la kuwapanga wajasiriamali kwa asilimia 100, lakini tuangalie tusitengeneze ufukara na umasikini wa kuwakandamiza na kuwakwamisha watu wetu,” alifafanua.
Shaka amesema amewaelewa vizuri kinamama hao ambao hawapingi kuhamishwa, lakini hofu yao ni pale walipohamishiwa kipato chao kinaweza kuwa endelevu.
“Nimemsikiliza mama anasema wamepangwa na wafanyanyibiashara ambao wao wanakuja kuwauzia wafanyabiashara wadogo kiasi kwamba pale pale hakuna anayetoa fursa kwa wanununuzi kuweza kunufaika.
“Kwa hiyo wenzetu wa serikali angalieni kiubinadamu, hawa wanatafuta riziki na ninyi mnasimamia sheria na taratibu, sasa hizo tararibu zisifike mahala tukatengeneza umasikini bila sababu,” alisema.
Aidha, Shaka amesema sehemu nyingi zilizo na vilio vya wamachinga hawalii kwa sababu wamehamishwa, bali wanalalamikia mazingira ya biashara katika maeneo walikohamishiwa kutokuwa rafiki.
“Chama kimesikia na wajibu wake ni kuishauri serikali na hapa tunashauri kuangaliwa mazingira rafiki ili wajasiriamali wafanye biashara zao. Hatuko hapa kwa ajili ya kutaka mrudishwe mlikokuwa hapana bali maeneo ambayo ni salama na rafiki kwa shughili zenu,” alisema.
Alisema Chama kitaendelea kusimamia maslahi ya wananchi kwa kuwa dhamira ya Rais Samia ni njema na anapenda kunyanyua mitaji ya wajasiriamali hususan akina mama.
DC AWARUDISHA WAFANYABIASHARA
Akizungumza kilio hicho cha wajasiriamali, Mkuu wa Wialaya Babati, Lazaro Twange, amesema lengo lilikuwa kuwawekea mazingira mazuri ya kuendesha shughuli zao za ujasiriamali.
Hata hivyo, alisema kutokana na changamoto zilizojitokeza amewaruhusu wafanyabiashara kurudi katika eneo la stendi ya zamani na kuwahakikishia serikali wilayani humo itawapa ushirikiano unaohitajika ukiwemo ulinzi ili wafanye shughuli zao kwa uhakika.
Aidha, aliwataka wananchi kuendelea kushirikiana na serikali katika kuleta maendelea ya wilaya hiyo ili ipige hatua zaidi za maendeleo.
Miongoni mwa malalamiko ya wajasiriamali hao ni pamoja na kufanya biaashar zao katika mazingira magumu, ikiwemo kutimuliwa na mgambo kila wanapopanga biashara.
Shaka alipongeza uamuzi wa mkuu huyo wa wilaya kuwaruhusu kinamama kuendelea na biashara zao kwenye eneo hilo, ambalo walionekana kulihitaji zaidi.
“Unaona hii ndio faida ya Chama kuishauri serikali, DC amesikia kilio na amelibeba, biashara zimeruhusiwa kufanyika usiku, wataimarisha ulinzi na usalama ili mwendelee na shughuli zenu usiku,” alisema.
Na MWANDISHI WETU, Babati



















