MKAZI wa Kijiji cha Mwamadulu, Kata ya Mwalukwa Mkoani Shinyanga, Madirisha Kanyalu, anadaiwa kumuua mkewe Evodia Nyerere (27) na mwanaye Meshaki Madirisha (11) kwa kutumia kitu chenye ncha kali na kisha kujiua kwa kujitumbukiza kwenye kisima cha maji.
Kauli hiyo imetolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Joseph Paul, alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusiana na tukio hilo.
Amesema tukio hilo lilitokea Machi 2, mwaka huu, saa 12:00 asubuhi katika Kijiji cha Mwamadulu mkoani humo.
Kamanda huyo amesema chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa kimapenzi, ambapo Kanyalu alikuwa akimtuhumu mke wake kuwa na uhusiano na wanaume wengine, ndipo Machi 2, mwaka huu, alitekeleza mauaji hayo kisha naye kwenda kujitumbukiza katika kisima cha maji kilichokuwa karibu na nyumba yake na kufariki dunia.
“Baada ya mauaji hayo kutokea miili yote ya marehemu hao ilifikishwa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Shinyanga kwa ajili ya uchunguzi, baadaye kukabidhiwa kwa ndugu zao kwa ajili ya taratibu za maziko,” alisema.
Kamanda huyo alitoa rai kwa wananchi mkoani humo kuyatumia madawati ya jinsia au ustawi wa jamii kupata suluhu la migogoro yao.
NA SALVATORY NTANDU, SHINYANGA



















