Na Angela Sebastian, Bukoba
JESHI la Polisi mkoani Kagera linaendelea kufanya uchunguzi wa tukio la vifo vya watu watatu wa familia moja ambalo limetokea Machi 26, mwaka huu, saa tisa usiku, huko wilayani Muleba.
Kamanda wa jeshi hilo mkoani hapa, Kamishna Msaidizi wa Polisi Revocatus Malimi, jana aliwataja marehemu hao ni Editha Martin (48) mkulima na binti yake, Pili Sawia (25) na baba wa familia hiyo, Sudi Mwamandi (49) ambaye anadaiwa kujinyonga baada ya kutekeleza mauaji ya mkewe na binti yake.
“Tukio hilo lilitokea katika Kijiji cha Mayondwe, Wilaya ya Muleba, ambapo Editha na Sawia walibadilisha dini yao ya mwanzo kutoka Uislam na kuwa Wakristo, jambo ambalo lilipingwa na mtuhumiwa na kusababisha kutokea ugomvi mara kwa mara.
Kutokana na ugomvi huo, Editha na Sawia walihama nyumba na kwenda kuishi sehemu nyingine.
Malimi alisema Machi 26, mwaka huu saa tisa usiku, ndipo mtuhumiwa alikwenda kwenye nyumba alipohamia mkewe na binti yake na kuvamia, akamkuta mkwewe peke yake na kuanza kumshambulia kwa kitu chenye ncha kali mwilini, kumkata kwa panga na kusababisha kufariki dunia.
Alisema na baada ya kutekeleza tukio hilo, alianza kukimbia kutoka eneo hili ndipo alikutana na binti yake njiani naye alimkata sehemu mbalimbali za miwili kwa panga na kupoteza maisha papo hapo.
“Kutokana na uchunguzi wa awali inaonekana baada ya kusababisha matukio hayo, mtuhumiwa alijitundika juu ya mti ulioko katika eneo hilo na kujinyonga kwa kutumia shuka…nawatahadharisha wananchi waache kabisa tabia ya kujichukulia sheria mikononi,” alionya.
Pia, alikemea tabia ya kuwanyanyasa wanawake kijinsia kwa kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaruhusu kila mtu kuabudu kwa imani anayoipenda.
Wakati huo huo, Kamanda Malimi alisema jeshi hilo linamshikilia Kusekwa Madaha (27) mkulima wa Kijiji cha Mulongo, wilayani Kyerwa, kwa tuhuma za kumpa mimba mwanafunzi wa darasa la nne (15).





























