WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso, amefanya mabadiliko kwa kuwaondoa watumishi sita katika nyadhifa zao, kwasababu mbalimbali za utendaji, uliosababisha kuzorota kwa huduma ya maji Wilaya za Newala na Nanyamba, Mkoa wa Mtwara.
Walioondolewa ni Mhandisi Primy Shirima ambaye ni Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi Mtwara (MTUWASA), Mhandisi Rejea Ng’ondya.
Wengine ni Mkemia Alualus Mkula (Mkuu wa Maabara ya Ubora wa Maji mkoa), Mhandisi Emanuel Konkomo (Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Makonde), Mhandisi Renard Baseki (Meneja wa RUWASA- Newala) na Anza Makala (Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Makonde).
Kwa mujibu wa taarifa ya wizara hiyo, wataalamu hao wa sekta ya maji watapangiwa majukumu mengine na wizara.
Katika hatua nyingine, Waziri Aweso amemwelekeza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, kuharakisha mchakato wa kumpata mkandarasi ambaye atajenga mradi mpya wa Makonde.
Mradi huo hivi sasa miundombinu yake imechakaa kutokana na kujengwa muda mrefu tangu miaka ya 1950.
Mapema Desemba, mwaka huu, Aweso alitia saini kibali cha kuanza utekelezaji wa mradi mpya wa Makonde.
NA MWANDISHI WETU





























