MJADALA kuhusu kupanda bei ya mbolea umetikisa Bunge, ambapo wabunge wameitaka serikali kueleza mikakati ya kunusuru sekta ya kilimo kwa kuhakikisha kunakuwepo mbolea na pembejeo za kutosha nchini.
Akichangia bungeni mjadala wa mapendekezo ya mwongozo wa maandalizi ya mpango wa bajeti ya serikali na mapendekezo ya mpango wa maendeleo wa taifa kwa mwaka 2022/23, Mbunge wa Singida Mashariki (CCM), Miraji Mtaturu, alisema serikali inapaswa kutenga sh. trilioni moja kuwekeza katika kilimo.
Alisema fedha hizo zitasaidia kupatikana kwa maofisa ugani wa kutosha na mbolea kwani bila kufanya hivyo kilimo hakiwezi kupiga hatua.
“Tupo kwenye nadharia zaidi hatupo kwenye vitendo, niombe serikali kama kweli tunasema tunataka kuwekeza tuhakikishe tunapata angalu trilioni moja iwekezwe kwenye sekta ya kilimo tuweze kupata maofisa ugani wa kutosha na mbolea ya uhakika,” alieleza.
Aliongeza: “Leo tunaongelea habari ya kilimo cha kutegemea mvua tunaambiwa wenzetu wa hali ya hewa wanatuambia tutakuwa na mvua chini ya wastani msimu unaokuja, je? mkakati umekuja vipi katika eneo hili,” alihoji.
“Mwanzoni mbolea ilikuwa inauzwa sh. 65000 lakini sasa hivi ni 120000 jambo ambalo hakuna mkulima anayemudu hivyo serikali chukueni jambo hili kwa dharura maana hali ni mbaya kwenye maeneo mengi,”alisema.
Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Subira Mgalu aliishauri serikali kuangalia changamoto ya kupanda kwa bei ya mbolea ili fedha zitengwe kwa ajili ya kuhakikisha mbolea inapatikana kwa bei nafuu.
Naye, Mbunge wa Muleba Kusini (CCM), aliishauri serikali ijitahidi kujenga kiwandaa cha mbolea hapa nchini haraka ili bidhaa hiyo ipatikane badala ya kusubiri kuagiza kutoka nje.
Alisema bidhaa hiyo ikizalishwa nchini itawezesha kupunguza uhaba wa mbolea ulipo ambao unaathiri maendeleo ya kilimo nchini.
Naye, Mbunge wa Viti Maalumu (CHADEMA), Stella Fiyao, alisema sekta ya kilimo ni muhimu kwa kuwa inachangia asilimia 26 ya ukuaji uchumi wa nchi, hivyo inatakiwa kupewa kipaumbele.
Mbunge huyo aliishauri serikali itumie njia ya dharura kwa dhumuni la kutatua changamoto ya upatikanaji wa pembejeo kwa wakulima.
Na SELINA MATHEW, Dodoma




























