CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeeleza kutoridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma ikiwamo ujenzi wa barabara ya Musoma-Mukojo-Busekela yenye urefu wa kilomita 92 kwa kiwango cha lami.
Mkandarasi wa barabara hiyo, amejenga kilomita tano tu huku kazi ya ujenzi ikisuasua ikiwa miaka mitano sasa tangu ujenzi huo uanze.
Mbali na ujenzi wa barabara, mradi mwingine ni ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo, ambao ulianza mwaka 2019 na mwaka 2021, Serikali ya Awamu ya Sita ikatoa fedha zote kukamilisha sh. Bilioni 1.49 zilizohitajika kukamilisha ujenzi ili ianze kutoa huduma ifikapo Agosti, mwaka jana.
Akizungumza wakati alipotembelea hospitali hiyo, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, amesema uzembe, urasimu na kukosekana kwa uhusiano na ushirikiano baina ya viongozi na watendaji ndani ya halmashauri hiyo, ni sababu ya kukwamisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Shaka ambaye alikuwa katika ziara ya Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa, iliyoongozwa na Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, alielekeza kufanyike ukaguzi maalumu wa miradi yote ya maendeleo ndani ya halmashauri hiyo, kwani kunaonekana huenda kuna mashaka.
“Kusuasua kwa miradi ya maendeleo ya wananchi ni sawa na kuihujumu serikali, kumhujumu Rais Samia Suluhu Hassan ambaye binafsi anatekeleza wajibu wake kwa kutoa fedha za kutekeleza wa miradi ya maendeleo,” alisema.
Shaka amesisitiza ukwamishaji wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025 ni kuikwamisha CCM na kumkwamisha Rais Samia, jambo ambalo Chama hakiwezi kukubali.
Aidha, amewataka viongozi na watendaji katika halmashauri hiyo, kujenga tabia ya kufanya kazi kwa ushirikiano na kuimarisha uhusiano mwema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Msogela Palela, alieleza sababu za kutokamilisha hospitali hiyo kwa wakati ni kukosekana kwa maji na eneo la ujenzi kuwa na mawe mengi, mambo ambayo Shaka aliyakataa kwa kuwa mita chache kutoka katika mradi huo, lipo Ziwa Victoria.
Na MWANDISHI WETU, Musoma





























