KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo, ameitaka Wizara ya Fedha na Wizara ya Kilimo kuhakikisha zinafanya uchunguzi kuhusu kupanda kwa bei ya mbolea nchini.
Chongolo ameyasema hayo leo jijini Dodoma katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika makao makuu ya CCM.
Ameeleza kwa sasa mbolea hiyo imepanda bei kufikia sh. 80,000 hadi 85,000 hivyo wizara hizo zinapaswa kufanya kila namna kuhakikisha bei inapungua ili kuwarahisishia wakulima.
Aidha, Chongolo amesema changamoto ya corona imesababisha viwanda vingi kushindwa kufanya kazi ya kuzalisha bidhaa hiyo kwa wingi, hivyo baada ya kufunguliwa na kuanza kufanya kazi, imeanza kupatikana.
Pia, Chogolo ameitaka bodi ya mazao mchanganyiko kuhakikisha soko la zao la mahindi linakuwa la uhakika kwa wakulima na kuhakikisha ununuzi wa mahindi kwa wakulima unaendelea hadi kufikia tani 100,000 ili nchi ijitosheleze kwa chakula.
Amesisitiza kuwa, bei elekezi ya ununuzi wa zao hilo kufika sh. 500 kwa kilo na iwe ni kwa wakulima wote nchini pasipo kuwaongezea kiasi kingine cha fedha kama fidia ya ushuru.
Na Benedict Mwasapi





























