DEREVA wa Kampuni inayojihusisha na usafirishaji wa mizigo mbalimbali (CRC) Wilfrerd Mnyenyerwa, amehukumiwa kifungo cha miezi 40 jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la wizi wa mafuta ya petroli lita 1,082.
Mnyenyerwa alipewa adhabu hiyo katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke mbele ya Hakimu Mkazi, John Ngeka.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Ngeka amesema mahakama imemtia hatiani mshitakiwa baada ya kujiridhisha na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka kwamba mafuta hayo yalisafirishwa na mshitakiwa mwenyewe kwenda Zambia na alitia saini upungufu wa mafuta hayo uliobainika.
Alisema mahakama hiyo iligundua kuwa mshitakiwa huyo alikabidhiwa mafuta lita 40,000 ili ayasafirishe kwenda eneo la Ndola, nchini Zambia, lakini alishusha lita 38,548 ambazo ni pungufu.
“Mahakama hii haina shaka mafuta yaliyokuwa yameshushwa na mashitakiwa alitia saini upungufu wa mafuta hayo,” alisema Ngeka.
Alisema mafuta hayo yalikuwa chini ya usimamizi wa mshitakiwa, hivyo anajua upungufu ulipotokea kwani alitakiwa ayafikishe kama alivyokabidhiwa.
Hakimu huyo alisema hakuna shaka kielelezo ambacho kilitiwa saini na mshitakiwa pamoja na Moses Kasekwa ambaye alipokea mafuta hayo huko Ndola, Zambia ambacho kiligongwa muhiri wa moto kilionyesha kuwa wahusika walipokea mafuta pungufu.
Alieleza kuwa mahakama hiyo ina imani kuwa mafuta hayo yalipakiwa sahihi na hayikuwa na upungufu, hivyo mshitakiwa ana hatia kwa kosa la wizi wa mali isafirishayo.
Alisema Kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakamani hapo,ilidaiwa kuwa mashitakiwa huyo alipakia mafuta hayo kutoka kwenye kituo cha Lake Oil kilichipo Kigamboni.
Ushahidi huo ulidai wakati mafuta hayo yanashushwa huko Ndola nchini Zambia, ilionekana kuna upungufu wa lita 1,082 na mshitakiwa mwenyewe alikiri kutokea hilo.
Alisema Kwa mujibu wa ushahidi huo , ilidaiwa kuwa kampuni huwa wanatoa risiti zao na wanayasafirisha mafuta hayo sehemu husika kwa kuwatumia madereva wao.
Mahakama ilimtaka mshitakiwa kujitetea kwanini asipewe adhabu kali, ambapo alidai kuwa ana familia inamtegemea na kosa hilo ni la kwanza anastahili kupunguziwa adhabu, hivyo mahakama ilimhukumu kwenda jela miezi 40 badala ya miaka 10 kama sheria inavyosema.
Inadaiwa kuwa Juni 29 mwaka 2020 maeneo ya Kurasini, Temeke Dar es Salaam ilipo Kampuni ya CRC, mshitakiwa huyo akiwa dereva, aliiba mafuta ya petroli yenye thamani zaidi ya shilingi milioni 3.8 mali ya kampuni hiyo.
Na REHEMA MOHAMED





























