WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalumu, Dk.Dorothy Gwajima, amezitaka kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto kuanzia ngazi ya kata kuongeza ubunifu na kuja na mfumo maalumu wa kusajili watoto wote katika maeneo yao na kuwafahamu wazazi wao ili kudhibiti ukatili na kuondoa wimbi la watoto wa mitaani.
Pia Dk.Gwajima, amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Kinodoni, Godwin Gondwe, kwa kushirikiana na watumishi wa Maendeleo ya Jamii na Ustawi kufanya mchakato wa haraka ili kudhibiti watoto ambao wanashinda barabarani na kuosha vioo vya magari katika Wilaya hiyo ikiwemo eneo la Mwenge.
Dk. Gwajima ameyasema hayo akiwa katika ziara yake ya kikazi alipotembelea ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, ambapo amesema kamati hizo zinajukumu la kujua watoto wangapi katika Kijiji au mtaa ambao hawaishi na wazazi wao na wangapi hawaendi shule ili kuchukua hatua.
“Kamati za Ulinzi Wanawake na Watoto zifanye usajili wa kutambua orodha ya watoto wote ili kujua yupi ni yatima ametoka wapi wazazi wake ni nani ili kudhibiti wimbi la watoto wa mtaani na kuzuia vitendo vya ukatili.
Watoto wengi wanatoka mikoani wanakuja Dar es Salaam tukifanikiwa Dar es Salaam tutakuwa tumefanikiwa, Mwanza na Arusha tutakuwa tumefanikiwa kuondoa wimbi la watoto wa mitaani” amesema
Dk. Gwajima ameongeza kuwa, kamati zikiwa hai na kufanya kazi ya kufuatilia kwa umakini Maendeleo na ustawi wa watoto kwa kushirikiana na viongoz wa dini itapunguza na kuondoa vitendo vya ukatili.
Vilevile Dk.Gwajima ameagiza kufanyika ufatiliaji wa haraka ili kubaini na kuwachukulia hatua watu wote wanaowatumikisha watoto.
Amesema watumishi wa maendeleo na ustawi kwa kushirikiana na kamati zitumie ubunifu wa kuwakusanya watoto na kuandaa matamasha mbalimbali ili kuweza kuongea nao na kujua changamoto wanazokutana nazo kutoka katika familia zao ikiwemo vitendo vya ukatili.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Godwin Gondwe, amesema wameshaanza kufanyia kazi changamoto hiyo kwa kushirikiana na maofisa Maendeleo ya jamii kwa kutoa elimu na kuangalia sheria inasemaje ili kuhakikisha watoto hao wanaondoka.
Gondwe amebainisha kuwa, uwepo wa watoto hao ambao hawasomi na badala yake wanafanya shughuli za kuosha vioo imekuwa ni changamoto kwa wananchi kwani baadhi yao wanalazimisa kufanya kazi hiyo na endapo mtu hatampa fedha mtoto huyo anamwagia uchafu jambo ambalo ni kero .
“Tumeshaanza kutoa elimu kulikuwa na watoto wanaomba omba lakini baadaye wanageuka na kuanza kuosha vioo na usipompa fedha huwa wanamwaga uchafu usiokuwa wa kawaida”alisema
Gondwe amesema watoto hao wengi wanatumia povu la maji na kusafisha vioo vya magari ambapo asilimia kubwa wapo eneo la Mwenge.
Amesema wanaendelea kufanyia kazi changamoto ya wimbi la watoto wanaozurura mitaani ambapo watakuja na mpango maalumu kama Wilaya ili kukabiliana na changamoto hiyo.
Na Mwandishi Wetu





























