MAKAMU wa Rais, Dk. Philip Mpango, amesema katika kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa chakula duniani, nchi za bara laa afrika zinaweza kufanya uwekezaji mkubwa katika kilimo na kutosheleza mahitaji ya chakula duniani.
Dk. Mpango amesema hayo wakati akizungumza katika mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani linalofanyika Davos nchini Uswisi alipochangia mada ya kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa chakula duniani.
Amesema nchi za Afrika kutokana na kujaaliwa ardhi na maeneo ya uzalishalishaji katika sekta ya kilimo, zinapaswa kuboresha sera ili ziwe rafiki katika kilimo kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za ukosefu wa chakula.
Aidha, Makamu wa Rais, ameongeza kwamba, nchi za Afrika zinapaswa kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji na himilifu, kuwekeza katika miundombinu ikiwemo barabara na kutenga ardhi kwa ajili ya kilimo cha mashamba makubwa na wawekezaji. Aliongeza kuwa, kutokana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi, kuna ulazima wa kuwekeza katika viwanda vitakavyozalisha pembejeo ikiwemo mbole na mbegu.

PICHA na O/Makamu wa Rais
Makamu wa Rais ameziasa taasisi za kimataifa za utafiti kuunga mkono jitihada za nchi za Afrika katika kuboresha afya ya udongo ili kuongeza tija na uzalishaji katika kilimo. Aidha, amesisitiza umuhimu wa suala la amani duniani ili kutoa fursa ya uzalishaji na usambazaji wa chakula duniani.
Aidha, Makamu wa Rais, amesema Tanzania inapanga kutumia rasilimali watu hasa vijana katika mnyororo wa thamani wa kilimo kwa kutenga maeneo ya kilimo yatakayo kwenda sambamba na huduma za pamoja kama vile huduma za ugani, pembejeo na masoko.
Mada hiyo imejadiliwa kutokana na dunia kukabiliwa na changamoto mbalimbali zinazosababisha upungufu wa chakula duniani kama vile Uviko-19, vita na mabadiliko ya tabia nchi.
Makamu wa Rais yupo Davos nchini Uswisi kumwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.
Na MWANDISHI WETU



























