WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Dk.Stergomena Tax amelitaka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kuwa wabunifu katika kupata raslimali fedha ili kukamilisha miradi ya ujenzi wa miundombinu ya uzalishaji kwenye vikosi vyake.
Waziri Dk. Stergomena ametoa maagizo hayo Wilayani Mlimba mkoani Morogoro alipofanya ziara ya kutembelea kikosi cha 837KJ Chita JKT kujionea miradi inayoendeshwa na jeshi hilo kupitia Mkakati wa Kilimo, Ufugaji na Uvuvi ikiwemo mradi mkubwa wa umwagiliaji ziara iliyokwenda sambamba na uzinduzi wa mradi wa ufugaji wa samaki.
DK.Stergomena amesema anatambua kuwa changamoto inayoikabili JKT ni raslimali fedha hivyo lazima wawe wabunifu katika kubuni miradi mbalimbali itakayowaingizia fedha ili waweze kujitegemea
Waziri huyo amehidi kwa niaba ya Serikali na wadhifa alionao kuwa ataendelea kusukuma ili JKT iweze kupata fedha za kukamilisha mradi huo wa umwagiliaji na ufugaji wa samaki na miradi mingine waliyonayo katika makambi mengine na watakayotaka kuianzisha .
“Hakikisheni changamoto mnazokutana nazo zisiwe kikwazo bali mzigeuze kuwa fursa za kujiletea mafanikio na kufanya Mambo makubwa zaidi na zaidi ninyi ni taasisi kubwa hapa nchini,”amesema
Pia ameishukuru Serikali kwa kulipatia Jeshi hilo kwa kutoa fedha kiasi cha Sh bilioni 3.5 fedha zitakazosaidia kuongeza vitendea kazi ikiwemo matrekta na vifaa vya kuvuna huku akisisitiza kuwa Serikali inatambua kazi kubwa inayofanywa na JKT.
DK.Stergomena amesema ukosefu wa mbegu za mazao mbalimbali ikiwemo mazao ya kimkakati imekuwa ni tatizo kubwa duniani na hivyo hatua waliokuja nayo JKT kuzalisha mbegu ni hatua ya kujivunia na kupongezwa.
“Hata kama mtu anamiradi mikubwa ya kilimo lakini hana mbegu itakuwa ni kazi bure kwa sababu atakuwa hana cha kupanda ingawa amelima mashamba makubwa,”amesisitiza waziri huyo.
Kuhusu vijana wanaojiunga na JKT, Dk.Stergomena aliwataka vijana wanaopata fursa ya kujiunga na JKT kutumia nafasi hiyo vizuri kwa sababu sio kila mtu anapata fursa ya kujifunza na kutumia mitambo ya kisasa ya kilimo, ufugaji na uvuvi.
Katika hatua nyingine waziri huyo amelitaka jeshi hilo kuhakikisha kuwa linazalisha zaidi chakula hasa ukizingatia Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini (TMA) imeshatangaza juu ya kuwepo upungufu wa mvua unaoweza kusababisha upungufu wa chakula nchini.
Akizungumzia miaka 60 ya uhuru, waziri huyo amesema jeshi lina jukumu la kuwajenga vijana kiuzalendo ili waweze kuwa vijana waliokamilika, ulinzi na uzalishaji.
Amesema miradi inayofanyika ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji katika kikosi hicho cha mafanikio JKT yaliyopatikana ndani ya miaka 60 tangu uhuru Tanzania Bara
“Mradi wa mwagiliaji ni mkubwa inaweza kwa kiasi kikubwa kulisha vijana wetu wa JKT. Kama mnavyofahamu usalama wa chakula ni kitu muhumu katika usalama,”amesema.
Pia amesema kuzalisha mbegu ni muhimu sana kwasababu huwezi kuzalisha mazao kama huna mbegu.
Amefafanua kuwa haya ni mafanikio ambayo yanahitaji miundombinu mbalimbali ambayo ni gharama kubwa sana ndio maana wakulima wanaanza wanaishia njiani.
Kuhusu mradi wa ufugaji wa samaki, Waziri huyo amesema mabwawa ya samaki yameanza ufugaji wa kitoweo hicho na kwamba lengo la kuzalisha tani 12 litafikiwa kwa haraka sana na hivyo kulisha nchi nap engine nje ya nchi.
Awai Mkuu wa JKT Meja Jenerali Rajabu Mabele amesema miundombinu inayojengwa katika kikosi hicho inahitaji fedha nyingi.
Meja Jenerali Mabele alifafanua kuwa hadi sasa mifumo ya umwagiliaji katika mashamba hayo imekamilika kwa asilimia 50 kwa kutumia fedha za kutoka vyanzo vyao vya ndani ikiwemo Suma JKT.
“Miundombinu hiyo imefanya kutumia takribani Sh4 bilioni na hivyo ili kukamilisha miradi hiyo inahitaji kiasi kisichopungua Sh bilioni 8, tunaimani waziri huyu anauwezo wa kuongeza fedha za kukamikisha kuwa mifumo hii inakamilika asilimia 100,”amesema mkuu huyo wa JKT.
Aidha, ameeleza kuwa wameanza kutumia maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji kwa kuingiza maji katika sehemu ya mashamba ya mbegu.
Mkuu huyo wa JKT amesema lengo la kulima mara mbili kwa mwaka masika na kiangazi na kwamba wakati wa kiangazi mazao yatakayopatikana yatakuwa mengi.
Amesema mazao yatakuwa mengi wakati wa kiangazi kwasababu watatumia maji kuingiza shambani kwa kiasi kinachotakiwa na kuyatoa yanapozidi na hivyo mbolea itakaa shambani tofauti na masika ambapo unaweza ukaweka mbolea ikaja mvua nyingi inaiondoa.
Na Happiness Mtweve,Mlimba





























