TANZANIA imeingia katika rekodi ya ongezeko la upatikanaji umeme, ambapo maeneo ya mijini umefikia asilimia 99.6 huku vijijini ukifikia asilimia 69.8.
Aidha, hadi sasa maeneo ya umma 15,200, taasisi za elimu 4,036, maeneo ya biashara 5,053 visima na mashine za maji 338, taasisi za afya 1,296 na nyumba za ibada 1,113, zimepatiwa umeme katika maeneo ya vijijini.
Akizungumza mafanikio na maendeleo ya sekta ya nishati katika miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba, alisema hadi Septemba mwaka huu, upatikanaji umeme umefikia Megawati 1,609.91 ikilinganishwa na Megawati 17.5 kabla ya Uhuru.
“Mahitaji ya juu ya umeme nchini yamefikia Megawati 1,273.42 Oktoba mwaka huu. Uwezo wa mitambo ya kufua umeme iliyoungwa katika mfumo wa gridi ya taifa umefikia Megawati 1,573.65.
Aliongeza kuwa: “Umeme wa nguvu ya maji (36.46%), gesi asilia (57.28%), Mafuta (5.60%) na Tungamotaka asilimia 0.67. Uwezo wa mitambo hiyo unajumuisha mitambo inayomilikiwa na TANESCO ambayo huchangia asilimia 86.57 na mitambo ya wazalishaji binafsi ambayo huchangia asilimia 13.43.”
Uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme iliyopo nje ya Gridi ya Taifa ni MW 36.26 ambapo TANESCO inamiliki mitambo yenye MW 31.26 na mzalishaji binafsi NextGen Solawazi (Kigoma) MW 5 kwa kutumia nguvu ya jua.
MRADI USAMBAZAJI UMEME DAR ES SALAAM
Mhandisi Mramba alisema serikali imekamilisha mradi wa kuboresha mfumo wa usambazaji umeme katika Jiji la Dar es Salaam.
Alisema mradi ulihusisha ukarabati wa Kituo cha Ilala kilovoti 132/33/11, ujenzi wa jengo Jipya la uongozaji la Ilala, ufungaji wa njia ya pili ya usafirishaji umeme wa Msongo wa kilovoti 132 kutoka Ubungo hadi Ilala.
Pia, alieleza mradi huo umehusisha kupanua kituo cha kupoza umeme cha Msasani kilovoti 33/11, ujenzi wa vituo vipya vinne vya kupoza umeme wa kilovoti 33/11 vya Jangwani Beach, Mwananyamala, Msasani na Muhimbili, ujenzi wa njia mpya za Msongo wa kilovoti 33 kutoka vituo vya kupoza umeme vya Makumbusho, City Centre na Tegeta kwenda vituo vipya vya Mwananyamala, Muhimbili, Jangwani na Msasani.
Kuhusu gridi ya taifa, Mramba alisema hadi Septemba mwaka huu, mikoa yote ya Tanzania Bara ilikuwa imeunganishwa katika gridi ya taifa isipokuwa mikoa minne.
Aliitaja mikoa hiyo ni Kigoma, Katavi, Rukwa na baadhi ya Wilaya za Mkoa wa Kagera ambapo mkoa huo unapata umeme kutoka nchi za Zambia na Uganda.
Alieleza kuwa baada ya serikali kusitisha matumizi ya mitambo ya kukodi ya binafsi ya kuzalisha umeme kwa kutumia mafuta mazito katika kuzalisha umeme ikiwemo ya Aggreko na IPTL, imeokoa wastani wa sh. bilioni 11.46 kwa mwezi.
Pia, alisema kusitisha uingizaji wa vifaa vya ujenzi wa miundombinu ya umeme zikiwemo nguzo, transfoma, nyaya na mita za LUKU na kuhamasisha uzalishaji wa vifaa vya kuunganisha umeme nchini, serikali imeokoa wastani wa sh. bilioni 162.57 kwa mwaka.
SEKTA YA MAFUTA
Mhandisi Mramba alisema mwaka 1996-2000, serikali ilianzisha taratibu za kuwa na soko huria katika biashara ya mafuta ili kuleta ushindani ambao utarahisisha upatikanaji na unafuu wa bei za mafuta na bidhaa zake.
Alisema pamoja na kuanzishwa kwa soko huria, bei za mafuta ziliendelea kupanda kiholela na kuleta adha kwa watumiaji.
Kutokana na hali hiyo, alisema mwaka 2006 serikali iliunda Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), kuanzishwa kwa Sheria ya Petroli ya mwaka 2015, kuanzishwa kwa Taasisi ya Mdhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), kuwepo kwa Kanuni za utekelezaji kama vile za Bei ya Gesi Asilia na Ushirikishwaji wa Wazawa.
Alisema usimamizi wa sekta umezidi kuimarika baada ya kuwepo sheria na kanuni hizo ambazo zimeandaliwa na kupitishwa ndani ya miaka mitano, kuanzia mwaka 2015 hadi 2020.
Aliongeza kuwa serikali iliweka mikakati ya kuhamasisha ushiriki wa wazawa katika shughuli za mafuta na gesi na hadi mwaka 2015 idadi ya wazawa iliongezeka maradufu katika kazi za utafutaji mafuta na gesi na uzalishaji wa gesi asilia.
Kwa mujibu wa Mhandisi Mramba, hadi Machi mwaka huu, mapato yanayotokana na mauzo ya gesi yamechangia zaidi ya sh. bilioni 208 katika Mfuko wa Mafuta na Gesi kuanzia mwaka wa fedha 2016/17 baada ya kukamilika ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka Mtwara/ Songosongo hadi Dar es Salaam.
Na FRED ALFRED, Dodoma





























