MFANYABIASHARA Anthony Magoe( 35), amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na mashitaka sita lkiwemo kujipatia sh. bilioni 1.3 kwa njia ya udanganyifu ili kuonyesha sampuli ya madini.
Magoe alifikishwa mahakamani hapoMei 16, 2022, na kusomewa mashitaka hayo na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Mwanga, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Godfrey Isaya.
Grace alidai kati ya Januari 18 na Februari 16, mwaka huu, maeneo ya jiji la Dar es Salaam mshitakiwa alijipatia dola za Marekani 602, 747 (sawa na sh. bilioni 1.3) kutoka kampuni ya Macbrusa Pyt kupitia akaunti iliyoko benki ya CRDB huku akijifanya ni za kuonyesha sampuli za madini.
Shtaka la pili, mshitakiwa anadaiwa Februari 9, mwaka huu, alighushi kibali cha kusafirisha madini cha sampuli chenye kumbukumbu namba 11000911 akionyesha kimetolewa na Wizara ya Madini.
Pia, anadaiwa Januari 19, mwaka huu, alighushi kibali cha kusafirisha madini kikionyesha kimetolewa na wizara hiyo na siku hiyo alighushi kibali cha maombi cha kusafirisha madini.
Wakili Grase alidaia Januari 9, mwaka huu, mshitakiwa alighushi risiti yenye kumbukumbu namba 920164000127430 akionyesha ni halali na kughushi nyaraka nyingine.
Mshitakiwa alikana mashitaka hayo, ambapo upande wa Jamhuri ulidai upelelezi umekamilika na kuomba shauri kuahirishwa hadi tarehe nyingine kwa kutajwa
Hakimu Isaya alitoa masharti ya dhamana yaliyomtaka mshitakiwa awasilishe fedha taslimu sh. milioni 750 au hati ya mali yenye thamani hiyo, awe na wadhamini wawili waaminifu wenye barua ya utambulisho kutoka serikali ya mtaa.
Mshitakiwa alikuwa na wadhamini wawili akiwemo mwenye hati ya mali isiyoamishika, lakini Mahakama iliahirisha kesi hiyo kwa muda ili hati iende kukaguliwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Na SYLVIA SEBASTIAN




























