MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abuobakari Kunenge, ameagiza kukamatwa kwa watu 16 waliohujumu miundombinu ya Mradi wa reli ya kisasa (SGR) na wengine walioiba mifuko ya saruji katika mradi wa ujenzi wa bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere.
Kunenge alitoa agizo hilo wakati alipoambatana na kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Pwani,wakuu wa wilaya, wenyeviti na wakurugenzi wa halmashauri za mkoa huo kutembelea mradi wa ujenzi wa daraja la Mto Wami.
Alisema kati ya watuhumiwa hao 16, watuhumiwa 11 wapo wilayani Rufiji.
Kutokana na matukio hayo, Kunenge aliagiza ulinzi uimarishwe zaidi katika maeneo ya miradi ya kimkakati.
“SGR ni mradi mkubwa na muhimu, unapaswa kulindwa, mradi huu unakwenda kuondoa msongamano wa magari na kupunguza ajali barabara kuu ya Morogoro-Pwani-Dar es salaam.
“Matarajio yetu treni ya umeme kuanza kazi Novemba, mwaka huu ili kunufaisha wananchi kwa kurahisisha usafiri na kufika kwa muda mfupi. Naomba jamii isaidie kulinda miundombinu ya mradi huu,” alisisitiza.
Naye, Mhandisi wa mradi huo,Tadei Kamu, alisema mradi huo wa SGR kipande cha Dar es Salaam- Morogoro, kimefikia asilimia 93.
Akiwa katika mradi wa daraja la Wami, Kunenge alimwelekeza mkandarasi kukamilisha ujenzi huo kwa wakati.
“Daraja la zamani halikidhi mahitaji ya magari yanayopita kwa kuwa lilijengwa miaka mingi iliyopita na ni jembamba lenye njia moja, barabara zinazounganisha daraja hili ziko katika miinuko mikali na kona mbaya ambapo ajali mbaya na vifo vimekuwa vikitokea mara kwa mara.
“Nimekuja na ninyi wote kwa kuwa ni timu moja ya mkoa ninayofanya nayo kazi mwone yanayofanyika chini ya serikali yetu ya Rais Samia,”alisema.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Chalinze (CCM), Ridhiwan Kikwete, alisema mradi huo umetengeneza ajira 500 za vijana, ambapo aliishukuru serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake.
Alisema daraja jipya likikamilika litakuwa kubwa lenye urefu wa mita 510 na upana wa mita 11.85 na linajengwa umbali wa mita 670 pembeni mwa daraja la zamani.
Ridhiwan alisema daraja hilo litakuwa na uwezo mkubwa katika usafirishaji na kufungua milango ya kimaendeleo na kukuza uchumi wa Chalinze na nchi kwa jumla.
Awali, akitoa taarifa ya mradi, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa Pwani, Andrea Kasamwa, alisema mradi huo umefikia asilimia 64.
Kwa mujibu wa Kasamwa, mkandarasi alianza kazi ya ujenzi Oktoba 22, mwaka 2018 ambapo aliwasilisha sababu za kimkataba za kuomba nyongeza ya muda wa ujenzi kufika mwakani.
Alisema tayari mkandarasi huyo ameongeza kasi ya kufanya kazi, ikiwa ni agizo la Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, ikiwemo kuongeza rasilimali watu kutoka 230 hadi 520, mitambo, mafundi na kufanyakazi mchana na usiku.
Na Mwamvua Mwinyi, Pwani





























