Na WAANDISHI WETU
WAKUU wapya wa wilaya, wametakiwa kuwa kiungo muhimu na wasimamizi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao.
Aidha, wametakiwa kuwa wasimamizi wa awali wa maagizo na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na viongozi wa juu hasa Rais Samia Suluhu Hassan ili kuharakisha upatikanaji wa maendeleo kwa wamanchi.
Maagizo hayo yalitolewa kwa nyakati tofauti na wakuu wa mikoa mbalimbali wakati wakiwaapisha wakuu wapya wa wilaya walioteuliwa hivi karibuni na Rais Samia ili kuanza kazi rasmi katika vituo vyao walivyopangiwa.
MOROGORO
Mkuu Mkoa wa Morogoro, Martine Shigella, amewaagiza wakuu wa wilaya kusimamia miradi yote ya maendeleo katika maeneo yao.
Kadhalika, amewaagiza wakuu wa wilaya ya Kilosa na Mvomero kwenda kusimamia mchakato wa kumilikisha ardhi ambayo hivi karibuni, umiliki wake ulifutwa na Rais Samia Suluhu Hassan, hivyo aliwataka igawiwe kwa makundi ya wakulima na wafugaji.
Vilevile, amewaagiza wakuu hao wa wilaya kuhakikisha wanaweka mpango, ratiba ya kusikiliza kero, matatizo na hata ushauri kutoka kwa wananchi na wadau mbalimbali.
Shigella pia amewata wakuu hao wa wilaya, kuhakikisha wanajenga sifa nzuri ya mkoa wa Morogoro, kwani licha ya mkoa kuwa na utulivu, bado kuna changamoto mbalimbali ambazo zinatia doa.
Wakuu wa wilaya walioapishwa katika hafla hiyo ni Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Halima Okash, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mjini, Albert Msando, Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Jabir Makame, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Majid Mwanga na Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Hanji Yusuph.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Msando amesema atahakikisha vyombo vyote vya kutoa maamuzi yakiwemo mabaraza ya ardhi ya kata na wilaya, yanajengewa uwezo ili yaweze kutenda haki.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Halima Okash, ameahidi kushirikiana na viongozi wa kata, vijiji na vitongoji ili kumaliza migogoro ya ardhi kwa kufuata sheria na miongozo.
KIGOMA
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye, amewaasa wakuu wake wa katika mkoa huo kufanya kazi kwa kufuata sheria, mipaka ya madaraka yao na kujenga mahusiano mema na wananchi.
Andengenye amesema hayo wakati akiwaapisha wakuu hao wa wilaya ambao wameteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, mwishoni mwa wiki iliyopita.
Amesema wakuu hao wa wilaya ni muhimu wakajenga mahusiano mema na watendaji wa serikali za mitaa ili kurahisisha utendajikazi wa mamlaka za serikali za mitaa na kusimamia ukusanyaji wa mapato ya serikali.
“Jambo ambalo nataka kusisitiza kwa wakuu wa wilaya kusimamia nidhamu ya mapato na matumizi ya halmashauri katika ukusanyaji mapato na matumizi, mwaka uliopita halmashauri sita za mkoa zimepata hati zenye mashaka kati ya halmashauri nane zilizopo, hivyo wakuu wa wilaya wana kazi ya kusimamia jambo hilo,” amesema.
Mkuu huyo wa mkoa aliwaonya wakuu wa wilaya kutojiingiza katika vitendo vya ubadhirifu, matumizi mabaya ya madaraka na kujilimbikizia mali kinyume cha sheria.
Akizungumza baada ya kuapishwa, Mkuu wa Wilaya Kigoma, Ester Mahawe, amesema wana jukumu la kusimamia mchakato wa maendeleo katika maeneo yao.
IRINGA
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Queen Sendiga, amezitaka halmashauri za wilaya mkoani humo, kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya wawekezaji ili kuondoa changamoto ya migogoro ya ardhi baina ya wawekezaji na wananchi.
Kauli hiyo ameitoa katika hafla fupi ya kuwaapisha wakuu wapya wa wilaya iliyofanyika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo.
Queen amesema migogoro mingi ya ardhi imekuwa ikisababisha wananchi kushindwa kuendelea na shughuli zao za kijamii kwa kuhofia uhai wao.
“Simamieni maeneo ambayo wawekezaji watawekeza kwa urahisi ili serikali iweze kuwapatia huduma wananchi,” amesisitiza.
ARUSHA
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela, amewataka wakuu wa wilaya sita za mkoa wa Arusha kufanya kazi ya kuwatumikia wananchi kwa sababu, mkoa huo una fursa nyingi za kuwakwamua wananchi kiuchumi.
Mongela ameyasema hayo wakati akiwaapisha wakuu wa wilaya wawili ambao ni Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Sophia Mjemba na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mhandisi Richard Ruyango.
Amesema Arusha bila majungu inawezekana na kwamba mkuu wa wilaya atakayendekeza majungu hataweza kufanikiwa kuleta maendeleo kwa wananchi.
“Tutasimamia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mpinduzi (CCM), hatupo tayari kusikiliza majungu bali tupo tayari kufanyakazi kuleta maendeleo kwa wananchi,” amesisitiza.
Akizungumza baada ya kula kiapo, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Sophia Mjema amesema yupo tayari kuleta maendeleo na mabadiliko katika wilaya hiyo kwa kuwatumikia wananchi usiku na mchana.
Amesisitiza kusimamia maagizo yote yanayotolewa na serikali kuanzia ngazi za juu kwa maslahi ya wananchi wa Wilaya ya Arusha.
Naye, Mkuu wa Ngorongoro, Raymond Mangwala, amemshukuru Rais Samia kwa kumchagua na kusisitiza kuleta maendeleo kwa wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mhandisi Ruyango ameomba ushirikiano kati yake na wananchi wa wilaya hiyo ili kuleta maendeleo, umoja na mshikamano.
MWANZA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, amewataka wakuu wa wilaya mkoani hapa kufanyakazi kwa weredi ili kukuza na kuongeza uchumi wa mkoa na taifa.
Akizungumza wakati wa kuwaapisha wakuu wa wilaya saba wa Mkoa wa Mwanza, amesema la msingi ni kuhakikisha uchumi wa nchi unaendelea kukua kupitia rasilimali zilizopo katika mkoa huo.
“Niwaombe tufanyekazi kwa mshikamano na weledi bila kubaguana, lakini pia tushirikiane kuongeza pato la Mkoa wa Mwanza kwa kutanua wigo wa uwekezaji katika maeneo yetu ya kazi,” amesisitiza.
Wakuu wa Wilaya walioapishwa ni Salumu Kalli (Mkuu wa Wilaya ya Magu), Johari Mussa (Wilaya ya Kwimba), Senyi Simon (Wilaya ya Sengerema) na Amina Makilagi ambaye ni mkuu wa Wilaya ya Nyamagana.
Wengine ni Hassan Elias (Mkuu wa Wilaya ya Ilemela), Denis Filangali (Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe) na Veronika Arbogast ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Misungwi.





























