WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amewaagiza wakuu wa mikoa na wilaya nchini, wafuatilie katika maeneo yao kuona kama kuna shule zinaendelea kuchangisha michango iliyozuiwa na serikali.
Pia, amewataka wazazi wote washirikiane na walimu kuweka mazingira mazuri ya kitaaluma ili wahakikishe watoto wa Kitanzania wanapata elimu bora.
Amesema hayo, alipokagua ujenzi wa madarasa ya shule ya Sekondari ya Babati Day iliyoko katika Halmashauri ya Wilaya ya Babati mkoani Manyara.
“Wazazi lazima tushirikiane na walimu ili kuhakikisha watoto wote waliofikia umri wa kwenda shule wanakwenda, ni marufuku kuwakuta wakifanya biashara. Mtoto lazima asome,”amesema.
Waziri Mkuu amemwagiza Mkuu wa Wilaya hiyo, Lazaro Twange, asimamie maboresho ya madawati katika shule hiyo kwa kuweka mbao badala ya mabati kama ilivyo sasa.
“…Madawati haya si mazuri yarekebishwe ili kuepusha madhara kwa watoto wetu. Marekebisho haya yanatakiwa yafanyike bila kuathiri mwenendo wa masomo kwa wanafunzi,” aliagiza.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwaondoa hofu wananchi wote kuhusu gharama za kuunganishiwa umeme vijijini kwamba itaendelea kuwa sh. 27,000.
Amesema wananchi hususan waishio vijijini hawahusiki na ongezeko la gharama za kuunganishiwa huduma ya umeme iliyotolewa hivi karibuni na Wizara ya Nishati.
Waziri Mkuu amesema malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, ni kuhakikisha vijiji vyote vinapata umeme ifikapo Desemba, mwaka huu.
Majaliwa amewataka wananchi hao waendelee kufanya maandalizi na malipo kwa ajili ya kuunganishiwa huduma hiyo katika makazi yao kwa kuwa ongezeko hilo haliwahusu.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amewahakikishia wananchi kuwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia inaendelea kusambaza huduma za maji.
Amesema hayo alipozungumza na wananchi katika kijiji cha Matufa baada ya kuweka jiwe la msingi la mradi wa maji wa Darakuta-Magugu utakaohudumia wananchi zaidi 80000.
Waziri Mkuu amesisitiza kwamba Serikali imedhamiria kufikisha huduma ya maji safi na salama katika maeneo yote nchini hadi vijiiini.”Endeleeni kuiamini Serikali yenu.”
Mradi huo una uwezo wa kuzalisha lita milioni 5.5 kwa siku, mpaka sasa ujenzi wake umefikia asilimia 95 na wananchi 45,000 wameanza kunufaika. Mradi huo umegharimu sh. bilioni 3.9.
NA MWANDISHI MAALUMU





























