WAZIRI wa Nishati, January Makamba, amevisisitiza Viwanda vya ndani vinavyozalisha vifaa vya umeme, kuongeza uzalishaji ili kukidhi mahitaji ya ndani.
Amesema kupitia mradi wa usambazaji umeme vijijini (REA), kutakuwa na mahitaji ya takriban Kilometa 340,000 za nyaya za kusambazia umeme mdogo na wa kati ili kufikisha katika maeneo yasiyo na nishati hiyo.
Waziri Makamba aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana, alipofanya ziara ya kutembelea kiwanda cha AFRICAB kinachozalisha nyaya, transfoma na vifaa vingine vya umeme nchini.
Aliusisitiza uongozi wa kiwanda kuhakikisha kinaendelea kuzalisha zaidi kwa kuwa serikali inatarajia kuharakisha miradi ya usambazaji umeme vijijini hivyo kutakuwa na mahitaji makubwa ya vifaa hivyo.
“Kutakuwa na mahitaji makubwa na ya haraka sana ya nyaya za ugavi wa umeme, sote tunafarijika kama serikali kwamba wapo wazalishaji wa ndani ya nchi kwa ajili ya kazi hiyo,” alisema.
Alieleza katika mradi huo wa REA hatua iliyopo sasa ni kusambaza umeme katika Vitongoji ambapo kati ya 64,000 vilivyopo nchi nzima ni 37,000 visivyofikiwa na nishati hiyo.
Alisema katika kipindi cha miaka minne ijayo watahakikisha wanamaliza vitongoji vyote na kazi hiyo itaambatana na mahitaji makubwa ya vifaa vya kusambazia umeme zikiwemo nyaya.
Alibainisha katika maeneo ambayo umeme haujafika ili ufike zinahitajika kilometa 122,000 za nyaya za umeme mdogo, kilometa 110,000 umeme wa kati na hivyo kufanya jumla ya mahitaji kuwa kilometa 340,000 za nyaya.
Kwa mujibu wa Waziri Makamba, mahitaji mengine ni tansfoma takriban 38,000 na yote yakikamilika karibunl wateja milioni tatu watafikiwa na umeme katika kipindi hicho.
“Kwa hiyo mtaona ni kazi kubwa inahitaji vifaa vingi vya bei nafuu na ubora unaostahili, tunafahamu kwamba kulikuwa na changamoto ya kupanda kwa bei ya Aluminiam duniani ambayo ndiyo malighafi na sisi hatuzalishi hapa nchini.
“Kwa sasa zimepungua na tunatarajia wenzetu AFRICAB watapata unafuu ili uzalishaji wa vifaa hivi usiathiriwe na kuongezeka kwa bei ya Alumuniam na Copper duniani,” alisema.
Alisema idadi hiyo ya kilometa za nyaya zitakazohotajika ni kwa ajili ya usambazaji pekee, bado kutakuwa na mahitaji ya nyaya za kuzalishia.
Kwa upande wake Ofisa Masoko wa Kampuni ya Kilimanjaro Cable inayomilikiwa na kiwanda hicho, David Tarimo, alisema wanazalisha vifaa mbalimbali vya umeme na ni kampuni ya wazawa.
Alieleza mbali na kiwanda kilichopo, kwa sasa wanaendelea na ujenzi wa kiwanda kingine kikubwa Kimbiji mkoani Pwani.
“Tuna imani hicho kitakidhi mahitaji ya vifaa vya umeme, kwani ni kikubwa pia kinatanuka katika uzalishaji, tunajivunia kuwa kampuni ya wazawa inayojali wazawa kwa kuwapa fursa,” alisema.
Aliipongeza serikali kwa hatua ya kuamua kutumia bidhaa zinazozalishwa ndani, kwamba hiyo imekuwa chachu kwao.
Na JUMA ISSIHAKA





























