BUNGE la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA), limeshindwa kuendelea na vikao vyake kwa madai ya kukosekana uwakilishi wa mawaziri wa nchi sita wanachama.
Imeelezwa kuwa mawaziri hao hawajahudhuria kwa muda mrefu, hivyo kukosa majibu ya rasimu zinazowasilishwa.
Wakizungunza katika kikao cha Bunge la nne linaloendelea jijini hapa, wabunge wa bunge hilo, walidai hawawezi kuendelea na kikao hicho kwa kuwa rasimu zinazowakilishwa zimekosa uwakilishi wa mawaziri au wawakilishi wao.
Mbunge Kenneth Muthioka kutoka Kenya, alisema kitendo cha mawaziri kukosekana katika vikao hivyo, kinasababisha malengo ya Bunge hilo kutotimia kwa wakati.
Ametolea mfano ripoti iliyokuwa iwasilishwe bungeni hapo kuhusu gharama za usafiri wa ndege kwa wananchi wa nchi za EAC ni kubwa na inahitaji majibu ya mawaziri, ili usafiri uwe wa gharama nafuu.
“Kwa mfano gharama za kutoka Nairobi kwenda Arusha kwa ndege ni ghali zaidi kuliko kutoka Nairobi kwenda Dubai,” amesema.
Mbunge Mariam Ussi Yahaya kutoka Tanzania, alisema kikao cha Bunge kilichokuwa kikijadili ripoti nne zikiwemo mbili zilizokuwa ziwasilishwe na mawaziri wenyewe na moja ya kamati ya hesabu zote zimekwama kwa sababu hawajahudhuria vikao.
Mariam amebainisha kuwa moja ya ripoti zilizokuwa zijadiliwe ni kuhusu suala la Sheria za Jumuiya ya Afrika Mashariki zinazopaswa zianze kutumika pia katika nchi wanachama.
“Hoja nyingine zilizokuwa zijadiliwe ni muswada wa usafiri wa anga kwa kutumia ndege ulioonekana ni wa ghali zaidi kwa nchi za Jumuiya hiyo, hivyo kuwaumiza wananchi wanaosafiri kufanya biashara na wanafunzi kwenda kusoma nchi wanachama,” alisema.
Amesema ripoti inaonyesha usafiri ndani ya nchi wanachama wa EAC ni ghali, jambo ambalo lilipaswa lijadiliwe mbele ya mawaziri na waamue namna ya kupunguza gharama za usafiri wa anga .
“Wabunge tunapaswa kuwasilisha hoja zetu ikiwamo ya usafiri huu ili wananchi wanufaike na Jumuiya yao. Tunataka mawaziri waone namna ya kupunguza gharama za anga kwa nchi za EAC,” alisema.
Spika wa muda wa bunge hilo, Abdulkadir Aden, aliahirisha kikao hicho hadi Machi mosi, mwaka huu, ambapo pamoja na mambo mengine Waziri mteule Betty Maina kutoka Kenya anatarajiwa kuapishwa ili awe miongoni mwa mawaziri wa EAC.
Betty ataapishwa baada ya waziri aliyekuwepo Aden Mohamed kujiuzulu kutokana na dhamira yake ya kugombea miongoni mwa nafasi za kisiasa katika uchaguzi mkuu wa Kenya unaotarajiwa kufanyika Agosti, mwaka huu.
Na LILIAN JOEL, Arusha





























