MWENYEKITI wa CHADEMA, Freeman Mbowe, amesema ana imani na Rais Samia Suluhu Hassan na Chama Cha Mapinduzi (CCM), ameiona nia njema iliyopo katika suala linalohusu maridhiano ya kisiasa nchini.
Mbowe alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na Wanadiaspora kupitia mtandao wa kijamii unaoitwa ‘Clubhouse,’ inayomilikiwa na raia wa Marekani, Paul Davidson.
“Nina imani sana na Rais Samia na serikali yake ya Chama chake, hadi sasa naona kuna dhamira njema.
“Nitakuwa mnyimi wa fadhila nisipokiri kuwa Rais Samia Suluhu Hassan, ameonyesha nia ya dhati kutafuta maelewano na upinzani,” alisema.
Kauli hiyo aliitoa wakati akijibu maswali ya wanadiaspora baada ya kuzungumza kwa kirefu kuhusu masuala mbalimbali yaliyohusu mwenendo wa chama chake na hali ya siasa iliyopo nchini.
Mbowe alisema baada ya kuitikia wito wa Rais Samia kwa ajili ya mazungumzo, baadhi wa watu wamempa ‘cheo’ cha ‘chawa’ wa Rais, huku wengine wakidai ‘amelambishwa asali’ ili kuendelea kuwa mtiifu kwa serikali.
“Siwezi kuwa chawa wa Mama Samia na wala mimi sio chawa wa Mama, lakini mnyonge mnyongeni haki yake mpeni, utawala wa Mama… ni tofauti sana, mtu yeyote mkweli ataona hilo,” alisema.
Alitumia fursa hiyo kuwataka vijana wa CHADEMA kuachana na mawazo ya kuingia barabarani kwa lengo la kufanya maandamano dhidi ya serikali, badala yake watoe nafasi kwa uongozi wao kuendelea na majadiliano na serikali.
Mbowe alisema matamanio yake ni kuona CHADEMA inaanza upya kwa kushirikiana na serikali na kusahau yote yaliyopita, ambayo alidai yamewaumiza kwa namna mbalimbali viongozi wa chama hicho kwa muda mrefu.
Alisema anaamini kwa umri wa miaka 60 alionao sasa, licha ya kuonekana mzee na wengine tayari wanamtambua kwa jina la Mzee Mbowe na akili yake bado ipo vizuri na muda ukifika ataachana na uongozi wa chama hicho.
Itakumbukwa kuwa, Mei 9, mwaka huu, Rais Samia alikutana na Mbowe Ikulu jijini Dar es Salaam, siku chache baada ya kiongozi huyo kuachiwa huru kufuatia yeye na wenzake watatu kufutiwa mashtaka ya uhujumu uchumi na ugaidi.
Baada ya mazungumzo hayo, Rais Samia alisema: “Kitu kikubwa tulichojadiliana ni kuwa, Tanzania ni yetu sote na tunapaswa kufanya kazi pamoja, kuijenga, lakini hili linawezekana tu iwapo tutajenga uaminifu na kudai haki, pamoja na kuheshimiana. Hii itatusaidia kupata nafasi ya kuijenga nchi yetu,”alisema.
MSIMAMO WA CCM
Mei 24, mwaka huu, CCM kupitia kwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, alisema Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama imepongeza, kuridhia na kuunga mkono Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Samia, kujadiliana na viongozi wa vyama vya siasa kwa lengo la kuimarisha demokrasia na maridhiano.
Shaka akizungumza na wanahabari alisema, CCM itaendeleza majadiliano ili kujenga jamii yenye usawa, uhuru wa kujieleza na kushiriki shughuli za kisiasa kwa kuzingatia maadili na sheria za nchi.
Na WILLIAM SHECHAMBO



















