RAIS Samia Suluhu Hassan ametoa Tsh. Bilioni 109 kwa ajili ya ujenzi wa shule za sekondari 234 ambapo kila jimbo litapata shule moja ambapo kila mbunge atapatiwa sh. milioni 470 za ujenzi wa shule hizo.
Pia, ametoa sh. bilioni 30 zitakazotumika kujenga shule maalumu 26 za wasichana katika kila mkoa ambapo kwa kuanzia fedha hizo zitatumika kujenga shule 10.
Akizungumza kuhusu mafanikio ya miaka 60 ya Uhuru ndani ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Waziri wa wizara hiyo, Ummy Mwalimu, alisema ujenzi huo utaanza mara moja.
Ametaja mikoa 10 ambayo itaanza kujengwa shule hizo ni Dar es Salaam, Mwanza, Songwe, Kagera, Lindi, Pwani, Ruvuma, Shinyanga, Singida na Tanga.
“…Katika hatua hii wiki iliyopita tumepeleka kiasi cha sh. bilioni 30 kuanza kujenga shule 10 za wasichana za masomo ya sayansi katika mikoa 10 ambapo kila shule itagharimu sh. milioni 600.
Ameagiza kuwa: “Ninaelekeza wakuu wa mikoa kuanza michakato ya ujenzi wa shule mara moja na kwa kuzingatia miongozo na taratibu zilizotolewa.”
Waziri Ummy alibainisha kuwa, serikali inaendelea na mpango wa kujenga shule mpya 1,000 za sekondari katika kata zisizokuwa na shule na ambazo zina msongamano mkubwa wa wanafunzi.
“Na katika hatua hii wiki iliyopita tumepeka kiasi cha sh. bilioni 109.9 kujenga shule 234 za kata katika majimbo yote 214 na shule 20 katika halmashauri ambazo zina shule zenye uwiano mkubwa wa wanafunzi darasani,” alieleza.

Alisema kila shule itagharimu sh. milioni 600, ambapo awamu wa kwanza zimepelekwa sh. milioni 470 kwa kila shule.
“Nitumie fursa hii kueleza kuwa, fedha hizi zitumike kuanza ujenzi wa madarasa nane, vyumba vya maabara ya masomo ya sayansi na matundu ya vyoo,” alisisitiza.
Pia, alisema serikali itajenga shule mpya za msingi ili kupunguza msongamano wa wanafunzi katika shule zenye wanafunzi zaidi ya 2,000 kwa lengo la kuwa na wastani wa wanafunzi wasiozidi 1,000 katika kila shule ya msingi.
Alisema kazi hiyo itakwenda pamoja na kujenga mabweni katika shule za msingi na sekondari ili kuwahudumia wanafunzi wanaotoka katika mazingira magumu na hatarishi na wenye mahitaji maalumu.
Pia, alisema serikali itaendelea kujenga na kukarabati miundombinu ya shule kongwe za msingi na sekondari ambapo kipaumbele kitakuwa ni kuboresha miundombinu ya shule kongwe za msingi zilizoazishwa kabla ya Uhuru.
MABORESHO USAFIRI WA UMMA
Kuhusu usafiri wa umma, Ummy alisema serikali itatunga sheria mahususi ya kuboresha usafiri wa umma katika miji yote kupitia miundombinu na huduma zilizoratibiwa.
Alisema lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha miundombinu na huduma hizo kuwa zenye ufanisi na endelevu kiuchumi, kijamii, afya za watu na mazingira.
Kadhalika, alisema utaanzishwa utaratibu wa kutenga na kuendeleza maeneo maalumu kwa ajili ya wafanyabiashara, wakiwemo wadogo na maeneo ya wazi ya umma.
“Kuongeza mabasi, idadi ya mbasi kwa awamu ya kwanza kutoka 210 yaliyopo sasa hadi 305 ifikapo Julai mwakani kwa awamu ya kwanza na kuleta mabasi yapatayo 755 kwa ajili ya kutoa huduma kwenye awamu ya pili ifikapo Machi 2023.
“Aidha, kuanza maandalizi ya kuongeza mabasi kwenye awamu nyingine hadi kufikia mabasi 3,650 yanayohitajika kwa awamu zote ifikapo mwaka 2025.” alieleza.
Na FRED ALFRED, Dodoma





























