TANZANIA imepokea dozi nyingine za chanjo za ugonjwa wa Uviko 19, zipatazo 500,000, aina ya Sinopharm kutoka China, huku serikali ikiweka hadharani mikoa 10 vinara kwa wananchi wake kuchangamkia chanjo zilizosambazwa awali.
Akizungumza katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere baada ya kupokea chanjo hizo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima, alisema chanjo hizo 500,000 aina ya Sinopham kutoka China zimepokelewa na kuthibitishwa ubora wake na watalamu wa ndani na nje kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO).
“Awali tulipokea chanjo aina ya Jonson&Johnson zipatazo milioni 1.58,400 na kufuatiwa na chanjo milioni 1,065,600, kutoka mpango wa COVAX Facility aina ya Sinopharm na sasa, tumepokea chanjo 500,000 za Sinopham lakini kutoka serikali ya China,”alifafanua.
Dk. Gwajima alisisitiza kuwa, chanjo aina Johnson zimeisha na Sinopham zilizoingia awamu ya pili, zilitumika katika kuchanja wananchi zaidi ya 88,546 hadi kufikia Oktoba 30, ambao ni zaidi ya asilimia 30 kati ya milioni 1.65 zilizoingia.
Alisema, hatua hiyo ni muendelezo wa kuwezesha wananchi kujikinga na ugonjwa huo, hivyo anatoa wito kwa mikoa kuchangamkia fursa hususan ambayo haifanyi vizuri kwa wananchi kuchangamkia chanjo.
MIKOA INAYOFANYA VIZURI KATIKA CHANJO
Aliitaja mikoa inayofanya vizuri kuwa ni Ruvuma, Kagera, Mbeya, Mtwara, Dodoma ambapo watu 7,000 hadi 10,000 wamechanjwa, ikifuatiwa na Arusha, Dar es Salaam, Mwanza, Mara na Songwe ambapo watu 4,000 wamechanja.
“Haya ni matokeo ya ujasiri wa Rais wetu Samia Suluhu Hassan, kwa wananchi wake ambao utakumbukwa kwa miaka mingi ijayo, hivyo ni vema mikoa ambayo haifanyi vizuri kuchangamkia fursa hii,”alisema.
Alisema, serikali itahakikisha inatoa chanjo katika vituo mbalimbali vya afya na wizara kutoa mwongozo, ili kufikia asilimia 60 ya Watanzania kupatiwa huduma hiyo.
Waziri Dk. Gwajima, alisema chanjo ni hiyari bila malipo kwa watu waliofikia miaka 18 na kuendelea, hivyo kutoa wito kwa jamii kujitokeza ili kupunguza makali ya mlipuko wa ugonjwa huo, vifo na idadi ya wagonjwa walio mahututi.
ATAKA ELIMU ZAIDI, BALOZI WA CHINA
Aliwataka viongozi wa dini, wasanii na viongozi wa vyama vya siasa kuendelea kutoa elimu ili kumaliza hatua ya utoaji wa chanjo kwa wananchi wote na kufanya ajenda nyingine za maendeleo.
Kwa upande wake Balozi wa China nchini, Chen Mingjian, alisema nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kulinda watu wake, hususan katika janga la ugonjwa huo wa Uviko 19.
“Ushirikiano baina ya China na Tanzania, ni imara kwa vizazi vijavyo na tutaendelea kushirikiana katika mapambano haya kwakuwa ni muhimu, ili kupata ukombozi wa kiuchumi na kijamii,”alisema.
Balozi Chen, alisisitiza kuwa ujio wa chanjo hizo kutoka nchini kwake, ni muendelezo wa ushirikiano huo katika mambo ya kijamii kwakuwa janga la Uviko 19 ni tishio la dunia nzima.
Na MARIAM MZIWANDA





























