NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM – Bara), Christina Mndeme, amewetaka wanachama kujipanga vyema na kujiandaa na uchaguzi ndani ya Chama utakaofanyika mwakani.
Amesema uchaguzi huo ni muhimu, ili kupata viongozi watakaomsaidia Rais Samia Suluhu Hassan, katika kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Mndeme ameyasema hayo katika vikao vya shina Namba Moja na Mbili wilayani, Ruangwa Mkoa wa Lindi, akiwa katika ziara ya wajumbe wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM, iinayoongozwa na Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo.
Ziara hiyo imelenga kuhamasisha uhai wa Chama kwa umma na kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025.
Aliwataka wanachama kujiandaa na uchaguzi bila kuwapo na mpasuko.
“Leo Rais amesema tumepata Rais mwanamke kwa kudra za Mungu na mfumo wa Katiba yetu, mwaka 2025 ndiyo tunaenda kuchagua Rais mwanamke, maandalizi yanaanza sasa ndani ya CCM, ikiwemo kuchagua viongozi wazuri kupitia uchaguzi wa mwakani,” alisema.
Alisema ni muhimu kamati za siasa na viongozi wa mashina, kukemea kuchafuana na kuweka mazingira rafiki ya ushindi wa CCM.
“2025 tunaenda na Rais Samia, tusikubali kupasuka, sumu haijaribiwi, tusiweke mazingira ya kuwapa wenzetu nafasi,” alisema.
Aliongeza, “hakuna haja ya kusikiliza wenye nia mbaya na taifa, serikali ikisema hivi wao wanageuka na kusema hivi, hawaridhiki,” alisema.
Pia, alisema ni vyema viongozi wa CCM wasifunge milango katika kuwasikiliza wananchi, kwa kutambua kuwa Ruangwa ina heshima yake, kwani ni jimbo linaloongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Pia, Mndeme alisisitiza ni wakati wa CCM kuhakikisha Chama, kinaheshimiwa na kutekeleza Ibara ya 251 ya Ilani, inayoelekeza kuwepo ukaguzi na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo ipasavyo.
Alihimiza haja ya kupokea wanachama wapya na kulipa ada, kuimarisha amani na kuwapo huduma muhimu kwa wananchi ikiwemo huduma bora za afya hususan kwa wazee.
Mndeme alisema Ibara ya 83 ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM, inaeleza umuhimu wa kuwapo afya bora na kuwa na dirisha la wazee kwa kuwa mchango wao ni mkubwa katika kutumikia taifa.
Mndeme alisisitiza wanachama na wananchi kujipanga kwa ajili ya maandalizi ya sensa itakayofanyika mwakani, kwa kuwa maendeleo yanahitaji takwimu sahihi ambazo zitapatikana kwa watu wake kuhesabiwa.
“Rais amezindua sensa, wakati ukifika tujitokeze, huwezi kusonga ugali wa watu watatu ndani kuna watu watano hawatashiba? Ni lazima kujua idadi na mahitaji yaliyopo na tujiepushe na wapotoshaji, tukahesabiwe,” alisema.
Na MARIAM MZIWANDA





























