RAIS Samia Suluhu Hassan, amewahakikishia Watanzania kuwa, moto katika kulinda madini hautazimika na kwamba serikali yake ipo macho kwa kila hatua itakayofanikisha nchi kunufaika zaidi na rasilimali hiyo.
Amesema hawezi kuruhusu uhujumu, wizi na utoroshaji wa madini, hivyo ameiagiza Wizara ya Madini kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, kuhakikisha hatua zinachukuliwa ikiwemo kufanya doria za mara kwa mara ili kuimarisha ulinzi.
Aidha, ameeleza kuwa, pamoja na kuimarika kwa udhibiti wa utoroshaji wa madini katika viwanja vya ndege, bandari na maeneo ya mipakani, anazo taarifa bado kuna utoroshaji wa madini katika baadhi ya maeneo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, katika utiaji saini makubaliano kati ya serikali na kampuni nne za uchimbaji madini, Rais Samia alisema mafanikio hayo ni safari ambayo hakuianza yeye, bali ilianzwa na mtangulizi wake, Hayati Rais Dk. John Magufuli na kusisitiza kwamba moto wa kulinda madini hautazimika kwa kuwa serikali yake ipo macho katika kila hatua itakayofanikisha nchi kunufaika na rasilimali hiyo.
“Serikali iliamua kufanya mabadiliko makubwa ya sheria zinazosimamia madini, ili kusaidia kumiliki rasilimali hizo kwa niaba ya wananchi na maslahi ya taifa,” alisema.
Rais Samia alisisitiza makubaliano yaliyofikiwa kati ya serikali na kampuni za uchimbaji wa madini, ni matokeo ya jitihada hizo kwa kuwezesha kuwa na ubia baina ya mwekezaji na serikali.
Aliongeza kuwa, miradi hiyo itaiwezesha serikali kupata tozo, ajira, gawio na ukuzaji wa huduma kwa kampuni na kurudisha hisani kwa wananchi.
“Ni wajibu wetu kuhakikisha shughuli za uchimbaji, uchenjuaji na uchakataji wa madini, zinasimamiwa vizuri. Hivyo wizara isimamie kikamilifu uongezaji wa thamani kwa kuwa haliepukiki. Leo kuna kampuni ilikuwa isaini hapa wakakataa kipengele cha uongezaji thamani, ninawapa wizara uwezo wa kusaini nao, lakini nisisitize tutachimba kuchenjua na kuongeza thamani hapa nchini,” alisema.
Rais Samia alisema hatua hiyo itasaidia fedha nyingi kubaki nchini na kwenda na mnyororo wa thamani.
Rais Samia alisisitiza sekta ya madini imeendelea kukua na kuongeza mchango wake katika pato la taifa, lengo ni kufikia mwaka 2025 sekta hiyo ichangia asilimia 10.
Alisema kutokana na hali iliyopo ambapo kwa sasa imefikia asilimia 6.7, ni wazi malengo hayo yatafikiwa.
Hata hivyo, Rais Samia alisisitiza kuwa na madini pekee si utajiri bali kuchimba, kuongeza thamani na kuchenjua, hivyo alifurahi kusikia wawekezaji walioingia mkataba wamekubali kupewa leseni na kuridhia kuhusu kuongeza thamani nchini.
Alisema ili kuhakikisha nchi inanufaika na rasilimali hiyo, ni vyema usimamizi na udhibiti wa madini katika viwanja vya ndege, bandarini na mipakani uimarishwe.
Rais Samia aliwataka waliopewa dhima ya kuzuia utoroshaji wa madini, kuwa wazalendo na kutokuwa chanzo cha utoroshaji.
“Nipongeze timu za majadiliano, haikuwa kazi rahisi, hata kuwa hapa si haba, mlikwenda mlishindwa mkarudi hadi kufikia leo, bado kuna mambo madogo madogo lakini kila yatakavyojitokeza mjitahidi kurudisha kwenye mstari,” alisema.

PICHA NA IKULU
UTOROSHAJI MADINI
Alisema pamoja jitihada hizo, zipo taarifa katika baadhi ya maeneo wahujumu kwa kushirikiana na watendaji wasiokuwa waaminifu, kunafanyika wizi hivyo aliwataka wanaosimamia wahakikishe hakuna madini yanayotoroshwa.
Rais Samia alisema kazi hiyo haiwezi kufanikiwa kwa kuachia vyombo vya dola pekee, bali wananchi watoe taarifa wanaposhuhudia mienendo isiyofaa.
“Vyombo vya ulinzi na usalama pia tulinde kila kona ili kuimarisha uchumi wetu, hali hii haikubaliki. Naigiza wizara kuongeza nguvu katika wizi na utoroshaji wa madini kwa kufanyika doria za mara kwa mara ili kujua wahusika na hatua zinaozchukuliwa,” alisema.
Alisema matarajio yake ni kuona makubaliano yaliyofikiwa utekelezaji wake unafanyika kwa haraka na kuleta manufaa kwa wananchi.
Alisisitiza kuwa kampuni hizo zitafanya uwekezaji wa zaidi ya sh. Trilioni 1.7 na kuongeza mapato jambo alilosema litatoa fursa za ajira, gawio na kuimarisha uchumi.
Rais Samia alieleza kuwa, miradi hiyo ikishirikisha wananchi ipasavyo wakati wa kupanga na kugusu maslahi yao itaondoa migogoro.
“Wasipokuwa na uelewa ndio matatizo yanaanza, nina taarifa kuwa mradi wa kuchimba mchanga Kigamboni una shida na wananchi wa Kigamboni hawapo hapa na walishaanza vurugu kupitia kwa diwani wao,” alisema.
Aliongeza kuwa ”Diwani huyo inamfanya kuwa na alama ya kuuliza kwa kuwa hata wakati wa operesheni ya Machinga ndio diwani pekee aliyehamasisha vurugu ili wasiondoke na sasa ameongoza tena wananchi kufanya vurugu kwa sababu hawajaelewa wakielimishwa wataulinda kwa kuwa mapato yatokanayo ndio watafaidika,”alisema.
AWAKUMBUSHA WAWEKEZAJI
Aidha, aliwakumbusha wawekezaji kuzingatia sheria, kanuni, miongozo na utunzaji wa mazingira hususan katika uchimbaji wa mchanga baharini.
Rais Samia alisema ni muhimu wasimamizi wa mazingira wakiwemo NEMC, wakaguzi wa uchimbaji na wawekezaji kuwa makini kwa kuwa, kusubiri madhara yatokee ili watoze faini na kukusanya fedha si malengo.
Alisema urudishaji wa fadhila kwa wananchi sio hiyari kwani ni haki yao, hivyo wahakikishe wanafikiwa ipasavyo.
“Wakuu wa wilaya, serikali za mitaa na wasimamizi acheni ubabe migodini sio mnaenda kuchukua fedha za fadhila kwa wananchi na kutumia kwa mambo mengine, lakini wabunge miradi hii ikawasaidie kujenga maendeleo ya nchi sio iwajenge nyie binafsi. Mambo ya kwenda kutisha kama si mimi msingepata kwa hiyo mimi nina ngapi hapana,” alisema.
Alisisitiza kuwa sera na sheria zimefanyiwa marekebisho kwa mtazamo wa kuvutia wawekezaji, hivyo anataka kuona wawekezaji wakubwa ambao watapandisha hadhi ya nchi wanafunguliwa milango.
Na MARIAM MZIWANDA



























