RAIS Samia Suluhu Hassan, ameanika neema sita zilizopatikana kwa Tanzania kutokana na ziara yake katika nchi za Ufaransa na Ubelgiji aliyoifanya hivi karibuni.
Amezitaja neema hizo ni kukwamua miradi iliyokwama, ukarabati wa Terminal II, Mabasi ya umeme kuanzishwa Dodoma/Dar es Salaam, uwezeshaji wa Afrika kutokana na athari za Uviko-19, fursa za mafunzo kwa Watanzania barani Ulaya na fedha za kukamilisha mradi wa mwendokasi na shughuli za kilimo.
Rais Samia alizitaja neema hizo, baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, akitokea Ufaransa na Ubelgiji alikokwenda kwa ziara ya kikazi.
Alisema ziara yake nchini Ufaransa aliifanya kwa mwaliko wa Rais wa nchi hiyo, Emmanuel Macron, ili kushiriki mkutano wa ‘One Ocean’ wenye dhamira ya namna ya kuzitumia bahari duniani kiuchumi na ulinzi.
Alibainisha kwamba katika mkutano huo walijadiliana kwa pamoja na kwamba bado mijadala mingine inaendelea ili kufikia mwafaka wa namna ambavyo ulimwengu unapaswa kufanya juu ya rasilimali bahari.
Alieleza pamoja na mkutano huo, akiwa nchini humo alifanya ziara ya kiserikali ambapo alikutana na Rais Macron na wafanyabiashara wa nchi hiyo.
Ukamilishaji barabara mwendokasi, kilimo
Akizungumzia neema hizo, Rais Samia alisema, “Tukiwa Ufaransa kama alivyosema Mkuu wa Mkoa (Amos Makalla) kuna vijipesapesa tumevipata pale kwa ajili ya kumalizia njia zetu za mwendokasi na tumepata pesa kwa ajili ya shughuli za kilimo”.
Mradi wa mabasi ya umeme Dar/Dodoma
Alieleza wakati wakijadiliana kuhusu mradi wa mwendokasi aliulizwa kwamba haiwezekani Dar es Salaam au Dodoma kukawa na mabasi ya kwenda kwa umeme.
“Nikawaambia inawezekana sana kwa hiyo hilo lipo katika mazungumzo na baadaye tutakuwa kama Ulaya miaka minne mitano, sita ijayo tutafika huko,” alisema.
Ukarabati Terminal II
Alisema akiwa nchini Ufaransa alitia saini mkataba wa ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Terminal II ambayo awali ilijengwa na Wafaransa, hivyo wamekubaliana watakuja kuifanyia ukarabati.
“Walivyosema itaishinda Terminal III, kwa hiyo mkataba tayari kampuni tumeshasainiana nayo karibuni watakuja na wataanza,” alisema.
Mafunzo
Alieleza akiwa nchini Ubelgiji alifanya mazungumzo na serikali na Umoja wa Ulaya (EU), ambapo katika serikali wamekubaliana kuwekeana mkataba katika suala la mafunzo.
“Nafasi za mafunzo zilikuwa zinatangazwa tu, watu wetu wanaomba 20 kwa Tanzania, lakini sasa tumewaambia ili tufuatilie vizuri tuwekeane mkataba nap engine idadi ya hizo nafasi izidi tunaendelea na mazungumzo mkataba tutasaidi baadaye,” alisema.
Mazungumzo na wafanyabiashara
Alisema katika nchi zote walifanya mazungumzo na wafanyabiashara na kutia saini mikataba kadhaa, kwamba chemba ya Tanzania na za biashara za mataifa hayo zilisaini ushirikiano.
“Hivi karibuni tunatarajia kupokea ujumbe wa wafanyabiashara kutoka Ufaransa na Ubelgiji waone wapi wanaweza kuja kuwekeza, imani yangu ni kwamba pale ambapo sekta binafsi inaweza kuwekeza serikali hatuwezi kuweka fedha yetu tutaitumia kwa mengine ambayo sekta binafsi haiwezi kuwekeza,” alisema.
Alisema bila kufanya hivyo Tanzania itachelewa kupata maendeleo na kufafanua kwamba msingi wa kuendelea haraka ni kushirikiana na wengine kama dunia inavyokwenda.
Kukwamua miradi iliyokwama
Kwa mujibu wa Rais Samia, kulikuwa na changamoto ya uhusiano na EU uliosababisha kukwama kwa baadhi ya miradi, ikiwemo Uwanja wa Ndege wa Kigoma, Shinyanga na Pemba na Miji ya Kijani ambayo ni Pemba na Kigoma.
“Kama mnavyojua katikati hapa tulichokozana kidogo na EU tulitetereka pesa za miradi zilikwama, lakini tumeshakwamua fedha za mradi mmoja umeshasainiwa na mwingine hivi karibuni kazi zitaendelea,” alisema.
Alisema katika mkutano wa Jumuiya ya Afrika (AU) na EU alioshiriki fedha Euro bilioni 150 zimetengwa kwa ajili ya Afrika.
“Hizo sasa ni kinyang’anyiro kwa Afrika atakayewahi mwanzo kupeleka miradi ya maana ndiye atakayepata fungu kubwa, kwa hiyo nasi tunajitayarisha tumeanza kupeleka michache tukiwa pale lakini tutajiweka vizuri tupeleke ili nasi tumege hilo fungu,” alisema.
Alibainisha kwamba katika mkutano huo walizungumzia masuala ya amani, usalama wa wahamiaji na ushirikiano wa kimataifa.
Uwezeshaji wa Afrika kutokana na Uviko
Kuhusu uwezeshaji wa Afrika kutokana na athari za Ugonjwa wa Virusi vya Corona (Uviko-19), alisema nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara zimetengewa Euro bilioni 55 ili kila taifa kwa wakati wake liende kuzungumza.
“Mazungumzo yangu nimevuna kama Euro 450 kwa miradi ambayo tutakwenda nayo kwa miaka mitatu,” alisema.
Alieleza katika ziara hiyo pia alikutana na baadhi ya watanzania wanaoishi nje ya nchi na kubainisha kwamba atayafanyia kazi maombi yote waliyoyawasilisha kwake.
“Kama mnavyojua sasa hivi tunafanya mapitio ya sera ya mambo ya nje na kipengele kikubwa ni kuwatambua ndugu zetu Watanzania walioko nje na kuwapa hadhi maalumu,” alisema.
Alisema sera hiyo ipo katika hatua za mwisho za marekebisho ili iwasilishwe serikalini, kisha bungeni kupitishwa na watanzania wanaoishi nje ya nchi kuanza kunufaika nayo ikiwemo kutambulika nchini.
“Kwa ufupi hayo ndiyo tuliyoyafanya pamoja na mengi mengine, lakini makubwa ndiyo hayo niwashukuru sana kwa mapokezi haya naomba mniruhusu sasa nikapumzike,” alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, alisema kilichofanywa na Rais Samia kimeijengea heshima Tanzania.
Alifafanua kwamba ziara ya Rais Samia imekuwa na mafanikio, ikiwemo upatikanaji wa fedha za kuendeleza mradi wa mwendokasi, Benki ya Kilimo na miradi mingine ya maendeleo.
“Wakati umeondoka Afrika Tour, wametuweka Dar es Salaam kuwa Jiji la sita linaloongoza kwa usafi,” alisema.
Akizungumza katika Uwanja huo, kabla ya Rais Samia kuwasili, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Dar es Salaam, Kate Kamba, alisema wamefarijika kuona harakati za Rais Samia za kuwaletea maendeleo wananchi.
Kate alisema ziara yake hiyo imeleta matunda kwa taifa ikiwemo kufanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali na kuwasihi watendaji wa serikali kutumia vizuri fedha watakazopewa kwa shughuli zinazokusudiwa.
Na JUMA ISSIHAKA



























