MWANASIASA mkongwe nchini, Stephen Wassira, amesema mgombea wa Urais wa 2025 kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni Rais Samia Suluhu Hassan pekee na sio mtu mwingine yeyote.
Pia, amewataka wenye nia ya kuwania urais mwaka 2025 kupitia CCM kuacha ndoto hizo kwa sababu utamaduni wa Chama ni kumuunga mkono rais aliyepo madarakani atimize miaka 10 ya kipindi cha uongozi kwa mujibu wa katiba ya nchi.
Wassira aliyasema hayo Februari 7, 2022, wilayani Bunda, Mara, baada ya Rais Samia kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa chujio la maji, ambapo alisema Rais Samia ameufanyia heshima kubwa mkoa huo kwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Alisema wenye kudhani wakisubiri miaka tisa hadi Rais Samia atakapomaliza uongozi wake kwamba watazeeka na wanataka kujitokeza 2025 kugombea wanapotea na waachane na ndoto hizo.
“Tunakupongeza na kukuhakikishia wananchi wa Mara kwa kazi unayoifanya, wanakuunga mkono na wale wanaosema wanautaka Urais mwaka 2025, ninawashauri wasubiri kwa sababu kwa utamaduni wa CCM kama una rais aliyeko ofisini huwa hatumpingi. Tunampa nafasi amalize kipindi cha awamu inayochukua miaka 10.
Aliongeza kuwa: “Kama wewe una umri mkubwa na ukifikiri ikipita miaka tisa utazeeka, basi acha maana hatuwezi kuwa maraisi wote. Maraisi ni kizazi. Mimi niliutaka sasa hivi siutaki tena kwa sababu umeshanipita, sasa wanakuja wengine. Kama wewe una miaka yenye mashaka usipoupata 2025 utachelewa ni bahati mbaya.”
Alimpongeza Rais Samia kwa kuupa heshima Mkoa wa Mara kwa kuleta maadhimisho ya miaka 45 ya kuzaliwa kwa CCM katika mkoa huo, ikiwa ni kumuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
AWESO
Kabla ya kumkaribisha Rais Samia kuzungumza na wananchi, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, alisema Rais Samia ni kiongozi wa kusema na kutenda.
“Tunamshukuru Mungu kwa sababu anaipenda Tanzania, nchi yetu tulipata mtihani wa kuondokewa na Hayati John Magufuli, lakini sasa tumempata Samia,” alieleza.
Aweso alisema Rais Samia ametoa fedha nyingi za kuhakikisha miradi ya maji inakamilika kwani katika wilaya ya Bunda mahitaji ya maji kwa wananchi ni lita milioni tisa lakini kiwango cha uzalishaji ni lita milioni tatu ambapo Rais ametoa sh. bilioni 10.9 kukamilisha mradi wa maji na wananchi wote watapata huduma hiyo kwa asilimia 100.
“Katika mji wa Shirati tumekamilisha mradi na sasa maji yanapatikana. Sirari wananchi walikuwa wakifuata maji nchi jirani, lakini umetoa fedha ambazo zimeanza kutumika kutekeleza mradi wa maji mkubwa kumaliza kero hiyo,”alisisitiza.
Alisema katika kuadhimisha wiki ya maji mwaka huu, ameagiza kila wilaya kutakiwa kuzindua mradi wa maji na siku hiyo haitokuwa ya kuvaa fulana na kofia bali kutathimini utendajikazi wa wizara katika kila eneo.
Vilevile, Aweso ambaye pia ni Mbunge wa Pangani (CCM), alisema kupitia fedha za Uviko-19 sh. bilioni 139 zilizotolewa na serikali, zinakwenda kutekeleza miradi ya maji 218 katika kila jimbo pamoja na kununua magari 25 ya kuchimba visima kwa kila mkoa kupata gari moja.
NA MUSSA YUSUPH, BUNDA




























