RAIS Samia Suluhu Hassan, amemteua Zuhura Yunus Abdallah, kuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Jaffar Haniu, kabla ya uteuzi huo, Zuhura alikuwa Mtayarishaji wa Vipindi na Mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).
Ilieleza kuwa, Zuhura anachukua nafasi ya Haniu ambaye atapangiwa kazi nyingine.
Uteuzi huo ulianza tangu Januari 30, mwaka huu.
Wakati huo huo, Rais Samia amemteua Uledi Abbas Mussa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) kwa kipindi cha miaka mitatu.
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Haniu alisema Mussa ni Katibu Mkuu Mstaafu na Mshauri Binafsi wa Masuala ya Kiuchumi wa Kimataifa (GFA Consulting Group), tawi la Tanzania.
Alisema Mussa anachukua nafasi ya Dk. Suleiman Magesa Misango ambaye ataendelea na majukumu yake ya Ukurugenzi ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na uteuzi huo ulianza Desemba 23, mwaka jana.




























