RAIS Samia Suluhu Hassan, ametangaza neema kwa wafanyabiashara wadogo ‘wamachinga’ ambapo amesema katika mwaka mpya wa fedha 2022/2023, serikali kupitia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) itatoa sh. milioni 10 kwa kila ofisi za machinga za mikoa.
Kauli hiyo aliitoa jijini Dodoma, alipopiga simu wakati wa mafunzo kwa viongozi wa Shirikisho la Umoja wa Machinga Tanzania (SHIUMA), yaliyoandaliwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
Rais Samia alipiga simu wakati, Naibu Katibu Mkuu wa SHIUMA, Joseph Mwanakijiji, akitoa changamoto walizonazo kwa serikali, ikiwemo uhaba wa maeneo ya kufanyia biashara, bima za afya, miundombinu ya masoko, bajeti na mitaji.
Wakati kiongozi huyo wa machinga akiendelea kueleza changamoto hizo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk. Dorothy Gwajima, alipigiwa simu na Rais Samia na kuiweka karibu na vipasa sauti ili washiriki wote wasikie.
“Nimesikia changamoto zenu mlizokuwa mnazizungumzia, naahidi kutoa sh. milioni 10 kila mkoa kwa ajili ya kuendeleza biashara zenu na kuwawezesha kufanya biashara kwenye mazingira rafiki na rahisi,” alisema.
Baada ya simu huyo, Dk. Gwajima alimshukuru Rais Samia kwa uamuzi huo, huku akiwasihi machinga wasikubali kurubuniwa na watu wasioitakia mema serikali ya Rais Samia.
“Acheni kutumika vibaya na baadhi ya watu wasio na nia njema na nchi, kwani tayari serikali inashugulikia changamoto zenu ili mfanye biashara katika mazingira rafiki,” alisema.
Aliwataka machinga hao kuwa mabalozi wa Sensa ya Watu na Makazi ili kazi hiyo ifanyike kwa ufanisi kama ilivyopangwa hususan katika halmashauri wanazotoka.
NA HAPPINES MTWEVE, DODOMA





























