MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge, amesema wamefanikiwa kutoa chanjo ya polio kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano kwa asilimia 122.
Aliyasema hayo katika kikao cha mkoa cha utekelezaji wa kampeni ya utoaji wa huduma za chanjo ya polio kilichofanyika mjini Songea, mwishoni mwa wiki na kuongeza kuwa, wamepata mafanikio makubwa katika awamu ya kwanza ya utoaji wa huduma hiyo.
Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Pololet Mgema, alibainisha katika awamu ya kwanza ya utoaji chanjo ya polio mkoa ulipanga kuchanja watoto 241,966, ambapo waliochanjwa ni 293,543 sawa na asilimia 122.
‘’Mkoa wa Ruvuma umekuwa kinara katika utoaji chanjo ya polio kati ya mikoa minne ya awamu ya kwanza iliyotekeleza kampeni. Pia, Mkoa wa Ruvuma ulikuwa kinara kwa utaoji chanjo za kawaida mwaka 2021,’’ alisisitiza.
Alisema katika chanjo ya Uviko-19 ambayo mkoa ulianza kuchanja Agosti, mwaka jana, walichanja watu 409,323 kati yao 322,363 sawa na asilimia 78.76 walikamilisha dozi na 86,960 walipata dozi ya kwanza.
Aliweka bayana kuwa ili kufikia asilimia 70 ya uchanjaji Mkoa wa Ruvuma, unatakiwa kuchanja watu 670,557 ambao ni asilimia 70 ya 957,938 wenye umri wa zaidi ya miaka 18 ya wenye sifa ya kupatiwa chanjo hiyo.
Mkuu wa Mkoa huyo, alieleza hadi kufikia Mei 15, mwaka huu, wamechanja watu 322,363 ambao walikamilisha dozi sawa na asilimia 48.07 ya 670,557.
Naye, Mratibu wa chanjo, Mkoa wa Ruvuma, Winbroad Mvile, alilitaja lengo la kampeni za utoaji huduma za chanjo ya polio ya matone kwa watoto chini ya miaka mitano ni kuzuia uwekezekano wa kupata madhara yanayotokana na virusi vya polio.
NA DUSTAN NDUNGURU, SONGEA



















