RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema katika kipindi cha ‘Royal Tour’ anachoendela kukifanya kuitangaza nchi kimataifa, kinahusisha kuionyesha dunia kuwa madini ya Tanzanite yanapatikana, yanachimbwa na yanauzwa kutokea Tanzania.
Rais Samia aliyasema hayo Septemba 5, 2021, alipofika wilayani Simanjiro mkoani Manyara, kuanza kurekodi kipindi hicho chenye dhamira ya kutangaza vivutio vya utalii, uwekezaji na biashara vilivyopo nchini. Alisema katika filamu hiyo, ataionyesha dunia kwamba chimbuko la madini hayo ni Tanzania na ushahidi wa namna yanavyochimbwa.
“Tutachukua filamu ndani ya migodi yetu, lengo ni kuionyesha dunia kwamba madini ya Tanzanite kwao ni Tanzania na tunakwenda kuwaonyesha ushahidi wa namna yanavyochimbwa, kuongezwa thamani na kuuzwa,” alisema.
Rais Samia alieleza kwamba katika kipindi cha nyuma madini hayo, yalikuwa yakizagaa katika mataifa mbalimbali kiasi kwamba ilikuwa ngumu kubaini kuwa yanatokea Tanzania.
“Nataka kuiambia dunia kuwa Tanzanite kwao ni hapa na haya madini yana mwisho, hivyo inabidi yachimbwe kwa mpangilio maalumu na kuuzwa kwa mpangilio maalumu, vinginevyo hatutaiona thamani yake,” alisema.
Alibainisha katika filamu hiyo, watakwenda mikoa mbalimbali kuonyesha vivutio vilivyopo, utawala bora na mazingira bora ili wageni wavutiwe kuwekeza au kutembelea nchini.
Aidha, aliwaahidi wakazi wa Wilaya hiyo kuwa, atapanga siku rasmi kwa ajili ya kufanya ziara ya kikazi. Alizitaja miongoni mwa changamoto wanazokabiliana nazo wakazi wa eneo hilo ni uhaba wa vituo vya afya, vyumba vya madarasa 91 na uhaba wa maji.
Alifafanua kuwa changamoto ya vituo vya afya na uhaba wa vyumba vya madarasa ipo katika hatua za kufanyiwa kazi, kupitia fedha zilizokusanywa kutokana na tozo za miamala ya simu.
“Kupitia tozo za miamala ya simu tutaanza kujenga vituo vya afya 220 kati ya 290 na Wilaya ya Simanjiro ni miongoni mwa zitakazonufaika, vyumba vya madarasa zaidi ya 500 vitajengwa nchini,” alisema.
Kuhusu maji, alisema tayari serikali imeshafanyia kazi ambapo kuna mabomba kutokea Arumeru yanaendelea kutandazwa kukabiliana na changamoto hiyo.
Aliahidi kutekeleza ahadi zote zilizotolewa wakati wa kampeni za uchaguzi na zilizopo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025.
Alisema baada ya kupatikana kwa eneo la hekta 250 katika mgodi huo, serikali itatoa fedha kujenga soko ili madini ya Tanzanite, yachimbwe, kuongezwa thamani na kuuzwa nchini.
“Serikali yenu inajipanga vyema, tunayajua matatizo naomba tushirikiane ili kutekeleza yanayotukwaza kwa sababu watu tunazaliwa kila leo, changamoto hazitaisha, lakini tutajitahidi kuzipunguza,” alisema.
Rais Samia alianza kurekodi kipindi hicho Agosti 30, mwaka huu na tayari ameshapita katika mikoa mbalimbali ikiwemo ya Zanzibar na Tanzania bara.
Katika hatua nyingine, alipokuwa Kilimanjaro, Rais Samia, aliahidi kufanya ziara katika mkoa huo Novemba, mwaka huu huku akisisitiza kuendelea na kazi ya utekelezaji miradi iliyoachwa na watangulizi wake.
Alisema anatambua changamoto zinazowakabili wakazi wa eneo hilo, hasa masoko na maji na kwamba serikali itatekeleza kama ilivyoahidi wakati wa kampeni za uchaguzi.
Rais Samia aliwataka wananchi kuchapakazi, kwa kile alichofafanua kuwa shughuli za ujenzi wa taifa hazipaswi kufanywa naye na wasaidizi wake pekee, inahitaji nguvu ya umma.
Na MWANDISHI WETU





























