MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mkutano wa kilele cha wiki ya UWT Taifa kumuenzi muasisi na mwanamke shupavu, Bibi Titi Mohammed itakayofanyika kesho, viwanja vya Ujamaa, Ikwiriri Rufiji.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Pwani, Mwenyekiti wa UWT Taifa, Gaudensia Kabaka amesema katika tukio hilo, wanatarajia kutembelea wagonjwa na kutoa vitu mbalimbali katika vituo vya afya na shule ya wasichana Ikwiriri.
“Tumeona mgeni rasmi awe Mwenyekiti wetu wa CCM Taifa, mwana UWT mwenzetu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani,”Tumeamua kuadhimisha kilele hicho Rufiji kwa sababu ya historia ya mama na mwanamke shupavu aliyemsaidia Baba wa Taifa Mwl.Nyerere kupigania Uhuru Bibi Titi Mohammed..
“Wiki ya UWT ilivyoanza ilianzishwa na chama cha TANU ilikuwa sehemu ya wanawake wa TANU na Mwl. Nyerere alikuwa akisaidiwa na Bibi Titi, ambaye alikuwa mhamasishaji mzuri ,muasisi na alikuwa Shupavu “
“Mwaka 1977 chama cha TANU na ASP vilipoungana, umoja ukaanzishwa UWT na mwenyekiti wake akaendelea kuwa Bibi Titi.”
Akielezea wiki hiyo, Kabaka alifafanua kuwa maadhimisho hayo yalianza Septemba 27 hadi Oktoba 4 kwa kujitangaza na kufanya shughuli mbalimbali, ambapo kauli mbiu ni “TUNAHUSISHA KUMKOMBOA MWANAMKE KIUCHUMI, KIFIKRA NA KISIASA.
Alisema mwanamke anapaswa kujikomboa kiuchumi kwa kusaidiana na baba kuwasomesha watoto wote bila kuwabagua.
Hata hivyo, Kabaka aliomba wanawake wajitokeze Rufiji kuadhimisha shughuli hiyo na kumuenzi Bibi Titi Mohammed huku wakiungana na Rais Samia ambaye atakuwa mgeni rasmi.
Kuhusu Rais Samia, sina haja ya kueleza ushupavu wake maana ameweza pia kutupatia trilioni 1.3 kwa ajili ya masuala mbalimbali ya kupambana na ugonjwa wa Uviko-19 pamoja na ujenzi wa madarasa na vituo vya afya.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge alisema pamoja na kuhakikisha sherehe hizo zinafanyika Pwani pia ni kumuenzi Bibi Titi Mohammed kwa ukombozi wake.
Alisema tukio hili litasaidia kuutangaza mkoa, kujua historia yake na kutangaza shughuli za utalii katika mkoa huo.
Kunenge alisema kuwa ni dhahiri Rais Samia anapita katika nyayo za Bibi Titi Mohamed kwa ushupavu wake hasa kwa jinsi anavyoipambania serikali kwa kusimamia miradi mikubwa yenye tija.
Aliongeza kuwa katika mkoa wa Pwani ipo miradi ya maji iliyopatiwa fedha kupitia DAWASA kwa maelekezo ya Rais Samia.
Ameelezea miradi mbalimbali inayoonyesha ushupavu wake kuwa ni mradi mkubwa wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere, mradi wa daraja jipya la Wami na mradi wa reli ya kisasa .
Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa kutokana na ushupavu alionao, wananchi wa Pwani wana kila sababu ya kumpenda Rais Samia kwa miradi mikubwa na ya kati inayoendelea .
Na MWAMVUA MWINYI





























