TUME ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Mionzi ya Nyuklia Kenya (KNRA), imeamuru shehena yenye namba TCKU3337296 iliyokuwa inaingia nchini ambayo ilibeba viasili vya mionzi ya nyuklia kurejeshwa ilikotoka.
Aidha, shehena hiyo ilikuwa katika meli MV SEAGO PIRAEUS VOY 174S ikisafirishwa (Transshipment) kuja Tanzania kupitia Bandari ya Mombasa.
Kupitia taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAEC Dk.Justin Ngaile, imesema kabla ya kuzuia shehena hiyo kurejeshwa ilikotoka, walipata taarifa kupitia vyombo mbalimbali vya Kenya, kuhusu shehena hiyo na kuwasiliana na KNRA ili kubaini ukweli.
“Tulipowasiliana na wenzetu KNRA kweli, Desemba 21, mwaka huu wenzetu walithibitisha taarifa hizo za kweli na tayari mamlaka ilichukua hatua stahiki na shehena kuamriwa kurejeshwa ilikotoka,”Imesema tarifa hiyo.
Kwa mujibu wa Dk.Ngaile, walipata taarifa Desemba 22, mwaka huu saa 6:30 usiku kuwa meli hiyo ilitia nanga nchini Oman katika Bandari ya Salalah.
Dk. Ngaile amesema TAEC imewaomba Watanzania kuondoa hofu kuhusiana na taarifa hizo, kwani shehena hiyo haikufanikiwa hata kuingia nchini.
NA LILIAN JOEL





























